Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wazee Wapewe Kipaumbele Katika Utoaji wa Huduma Za Kijamii
May 24, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Ismail Ngayonga

SERA ya Taifa Wazee Tanzania ya mwaka 2003 inaeleza kuwa Mzee ni mtu mwenye umri wa miaka 60 na zaidi.

Katika baadhi ya nchi za Afrika zipo imani mbalimbali potofu juu ya wazee, hii hupunguza uthamani wao ndani ya jamii hata ushiriki katika mambo ya maendeleo.

Idadi ya wazee inazidi kuongezeka duniani, takriban watu milioni 700 au asilimia 10 ya idadi ya watu duniani wana umri juu miaka 60, na ifikapo mwaka 2030, kutakuwa na watu wengi wenye umri zaidi ya miaka 60 kuliko watu wenye umri chini ya miaka 10.

Takwimu ya Sensa ya Taifa ya mwaka 2012 zinaonesha kuwa Tanzania ina idadi ya wazee 2,507,568 sawa asilimia 5.6 ya Wananchi wote, ambapo ni tofauti na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002 iliyoonyesha idadi ya wazee kuwa asilimia 4.0, hivyo kufanya idadi hiyo kuongezeka kwa kiwango cha asilimia 1.6.

Ongezeko hili linaonekana zaidi katika nchi zinazoendelea ambapo viwango vya ongezeko hilo havilingani na uwezo wa rasilimali zilizopo kuwahudumia katika nyanja za afya, lishe na huduma nyingine za msingi kwa maisha ya binadamu.

Maslahi ya waze  yamezungumzwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambapo inatamka wazi kuwa wazee kupewa heshima na kupata hifadhi kutoka serikalini na kwa jamii kwa ujumla.

Tangu mwaka 2002 Nchi yetu ilipoungana na Nchi nyingine duniani kutia saini Mkataba wa Kimataifa wa Wazee ilikuwa ni kielelezo tosha cha nia njema ya kuendelea kuboresha na kuendelea kubuni na kuweka mipango mbalimbali yenye lengo la kuboresha maisha ya Wazee.

Pamoja na matamko haya, hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa kuboresha maslahi ya kundi hili muhimu na lenye hazina kubwa, bado Serikali na wadau wengine wa maendeleo wanapaswa kuongeza juhudi kuboresha utoaji wa huduma kwa wazee.

Wazee ni kundi ambalo limeonekana kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kuathirika, kwani wengi huzeeka na kuwa na afya dhaifu kutokana na maisha  na magonjwa ya mara kwa mara na ya muda mrefu, ni hali ya kawaida kwa wazee walio wengi.

Pamoja na ukweli huo huduma za afya hazipatikani  kwa urahisi kwa wazee walio wengi na mara nyingi huduma hizo ni ghali. Pia watumishi wa afya wanaohudumia wazee hawaonyeshi  mwamko na hawana mafunzo ya kutosha katika eneo hili la huduma.

Aidha wazee walio wengi hasa wa vijijini wanaachwa nje ya utaratibu wa kupata huduma kutokana na kushindwa kuthibitisha kwamba wana umri wa miaka 60 na hawana uwezo wa kuchangia gharama hizo.

 Akiwasilisha Hotuba ya makadirio ya bajeti ya mwaka 2016/17, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu anasema  Wizara imeendelea kuratibu utolewaji wa huduma za matibabu bure kwa wazee, ambapo imeagiza vituo vya kutolea huduma ya afya katika Halmashauri na Mikoa na rufaa kutenga  dirisha maalum kwa ajili ya matibabu ya wazee.

Anaongeza kuwa Hadi kufikia machi 2016 jumla ya madiridha ya wazee 24 katika hospitali za mikoa na 133 katika hospitali yametengwa kwa ajili ya matibabu ya wazee.

“Wazee ni hazina, hivyo Wizara inaelekeza uongozi wa vituo vya afya vya umma siyo tu kutenga dirisha la wazee bali kuweza sehemu maalum ya kutoplea huduma kwa wazee ili kuwapunguzia usumbufu” anasema Waziri Ummy.

Kwa mujibu wa Waziri Ummy anasema Wizara ya Afya kwa kushirkiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI imeendelea kuhamasisha halmashauri kuweka utaratibu wa kuwakatia Bima ya Afya ya Jamii (CHF) , ili kupunguza changamoto za upatikanaji wa huduma ya afya kwa kundi hilo.

Aidha anaongeza kuwa Wizara pia imekusudia kuandaa mkakati wa kuboresha huduma za afya kwa wazee, itaboresha upatikanaji wa takwimu zinazohusu wazee katika ngazi zote za kutolea huduma, itahakikisha kuwa dawa zinazotakiwa kutibu magonjwa yanayowasibu wazee mara kwa mara.

Serikali imekuwa ikitekeleza programu mbalimbali ikiwa ni kielelezo tosha cha nia njema ya kuendelea kuboresha na kuendelea kubuni na kuweka mipango mbalimbali yenye lengo la kuboresha maisha ya Wazee.

Katika kipindi cha mwaka 2013/2014 jumla ya wazee 1,226 walipatiwa huduma muhimu za kujikimu; kama chakula, afya na malazi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera yaTaifa ya Wazee ya mwaka 2003 na Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010.

Ni wazi kuwa Serikali imejitahidi kuhakikisha wazee wanaandaliwa mazingira rafiki kwa kutambua uwezo mkubwa wa kujitolea, kujali, wenye huruma, kushauri, kuongoza na kushiriki katika mambo yanayo ihusu jamii.

Wadau wa maendeleo wanapaswa kuongeza juhudi kuboresha utoaji wa huduma kwa wazee na kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kikamilifu.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi