Na Fatma Salum
Serikali imewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuwakamata na kuwashitaki mahakamani watoto pamoja na wazazi wao ambao huzagaa mitaani kuombaomba.
Agizo hilo limetolewa leo bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Joseph Kakunda, wakati akijibu swali la Mbunge wa Kiembesamaki, Ibrahim Raza, lililohoji ni lini Serikali itachukua hatua ya kuwaondoa ombaomba Jijini Dar es Salaam.
Kakunda alibainisha kuwa ni kweli ombaomba wengi zaidi wapo Jijini Dar es Salaam kutokana na kuwepo kwa vivutio vingi ikiwemo watu wenye imani mbalimbali ambao wengine huwapatia fedha ombaomba hao kama sehemu ya ibada.
“Kuzagaa kwa ombaomba kimekuwa chanzo kimojawapo cha uchafuzi wa mazingira na mara kadhaa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam imechukua hatua mbalimbali za kuwaondoa ikiwemo kuwakamata na kuwarudisha kwao lakini wamekuwa wakirudi,” alisema Kakunda.
Alieleza kuwa mwaka 2013 ombaomba wapatao 253 na watoto 135 walikamatwa na kurejeshwa kwao ambapo watoto 33 walirejeshwa shuleni, hivyo inathibitisha kwamba wapo watu wazima wanaowatumia watoto kuombaomba na kuwakosesha fursa ya kupata elimu au kuwa watoro.
“Nawaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri chini ya usimamizi wa Wakuu wa Mikoa kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama, kuwakamata watoto wote ambao badala ya kwenda shuleni huzagaa mitaani kuombaomba,” alisisitiza Kakunda.
Alisema kuwa watoto hao wakamatwe pamoja na wazazi wao na washitakiwe mahakamani chini ya Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 inayokataza utoro na Sheria ya Kanuni ya Adhabu kifungu cha 166, 167 na 169 (a) vinavyohusu Wajibu wa Wazazi na Walezi kwa Watoto.
Pia Kakunda alishauri Mabaraza ya Madiwani kutunga sheria ndogondogo za kuzuia utoro pamoja na kudhibiti mienendo ya baadhi ya watu wanaoombaomba.
Aidha, alitoa rai kwa watanzania kutumia fursa za kupambana na umaskini zilizoandaliwa na Serikali ikiwemo elimu ya msingi bila malipo, huduma za afya vijijini, fursa za mikopo na matumizi bora ya ardhi yenye rutuba ili waweze kujikwamua kiuchumi.