Na: Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma.
Serikali imeshauri Wazazi/Walezi kuchagua Shule kulingana na uwezo wa kulipa ada kutokana na tofauti ya viwango vya ada na huduma zitolewazo kwenye shule binafsi.
Ushauri huo umetolewa leo Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. William Tate Ole Nasha alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Mariam Nassor Kisangi juu ya kwa nini Serikali isikae na wadau husika ili kupanga ada elekezi kwenye shule binafsi.
"Serikali haitajihusisha na upangaji wa ada kwa shule binafsi, bali itaendelea kusimamia viwango vya ubora, taratibu, kanuni na sheria za uendeshaji wa shule zote nchini," amesema Mhe. Ole Nasha.
Ameendelea kusema, lengo la Serikali ni kuhakikisha watoto wote wa Kitanzania wanapata elimu bora kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.
Aidha amesema, Serikali inatambua na kuthamini mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya elimu nchini ambapo hadi sasa, jumla ya shule ya msingi 1,432 kati ya shule 17,583 zinamilikiwa na sekta binafsi.
Amesema jumla ya shule za Sekondari 1,250 kati ya shule 4,885 zinamilikiwa na sekta binafsi. Vile vile Serikali inatambua utofauti wa viwango vya ada kati ya shule za umma za shule binafsi pamoja na utofauti wa viwango hivyo kati ya shule moja na nyingine za binafsi.