Frank Mvungi- Maelezo, Dodoma
Serikali imetoa rai kwa wawekezaji kujitokeza kuwekeza katika viwanda vya kuchakata samaki, madini ya chokaa na michikichi ili kuchochea ukuaji wa uchumi na Ustawi wa Wananchi na Taifa kwa Ujumla.
Akizungumza katika Kipindi cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Mkuu wa Mkoa huo Brigedia Jenerali (Mstaafu) Emmanuel Maganga amesema kuwa Mkoa huo una mkakati wa kuanzisha viwanda vitatu (3) mpaka vitano (5) vya kuchambua pamba na katika kipindi cha miaka miwili kutakuwa na viwanda vya kutengeneza bidhaa za pamba.
“Kichocheo Kikubwa cha maendeleo ni kuwepo kwa miundombinu ya barabara za lami,Reli na Bandari ambapo kwasasa Serikali inajenga barabara kutoka Nyakanazi hadi Kigoma, Kigoma hadi Tabora, Kigoma hadi Mpanda”
“Pia mpango wa Serikali wa kuifikisha reli ya kisasa (SGR) hadi Kigoma na maboresho ya badari, hii ni nia njema ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuuletea maendeleo katika Mkoa wa Kigoma hali itakayosaidia katika utekelezaji wa dhana ya ujenzi wa uchumi wa Viwanda” Alisisitiza Brigedia Jenerali Maganga.
Akifafanua kuhusu upatikanaji wa nishati Brigedia Maganga amesema kuwa maeneo ambayo hayakupata umeme katika awamu zilizopita za mradi wa REA, sasa mradi wa REA awamu ya III utayafikia maeneo hayo ili kuchochea kasi ya ukuaji wa maendeleo.
Aliongeza kuwa kwa kushirikisha wadau katika sekta ya uvuvi ikiwemo kutengeneza mtambo ya kutengeneza barafu ili kuwezesha samaki wanaovuliwa kukaa kwa muda bila kuoza ili kuongeza tija kwa wavuvi.
Pia alitoa wito kwa Wakazi wa Kigoma tuendelee kuchapa kazi, tushikamane tusirudi nyuma katika uzalishaji ili kulinda sifa ya Mkoa huo ambayo ni kutokukumbwa na baa la njaa tangu Taifa letu lilipojipatia uhuru.
“Nilipofika Kigoma tuliamua kutekeleza kilimo cha kiwango cha kati kwa kuanzisha vituo vya matreka, dhumuni ni kupanua wigo wa kilimo.” Alisisitiza Brigedia Maganga
Aliongeza kuwa Mkoa una maafisa Ugani na wamepewa maelekezo mahususi kuhusu usimamizi wa maeneo yanayotekeleza shughuli za kilimo badala ya kukaa maofisini.
Akizungumzia suala la Wakimbizi Brigedia Maganga amesema kuwa katika kipindi cha hivi karibuni wakimbizi 13,000 wamerejeshwa nchini Burundi kwa hiari baada ya hali kuwa shwari katika Taifa hilo.
Tumekubaliana na Balozi wetu nchini Congo kuwa mwezi huu tufanya ziara ya pamoja katika mji wa Kalemie hasa kuangalia masuala muhimu ikiwamo ya kibiashara kwani mkoa wa Kigoma ni moja ya mikoa ya kimkakati kwa maana ya shughuli za kibiashara.
Katika suala la Afya tumetilia mkazo katika suala la afya ya mama na mtoto na tuna vituo 27 vinavyofanya kazi na vinafanya upasuaji mdogo na mkubwa.
Kipindi cha TUNATEKELEZA kinarushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kuratibwa na Idara ya Habari MAELEZO, Awamu iliyotangulia iliwashirikisha Mawaziri wote na Awamu hii ni Wakuu wa Mikoa.