Na Munir Shemweta, DODOMA
Watumishi wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi wameanza kupata chanjo ya Uviko- 19 katika ofisi zake zilizopo Mtumba katika Mji wa Serikali mkoani Dodoma.
Wataalamu wa sekta ya afya kutoka jiji la Dodoma wakioongozwa na Daktari wa Jiji Revocatus Kitena ndiyo waliokuwa wakiendesha zoezi la kuchanja watumishi wa sekta ya ardhi Makao Makuu Mtumba leo tarehe 28 Sept 2021 ikiwa ni jitihada za kuhamasisha watumishi kuchanja kujikinga na ugonjwa wa Corona.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Zakariya Kerra alisema zoezi hilo la chanjo ya Uviko -19 litafanyika kwenye ofisi zote za Makao Makuu ya Wizara na nyingine kwa wale watumishi ambao hawakupata chanjo.
‘’Watumishi wote ambao hawakupata chanjo sasa wanaweza kupata chanjo ya Uviko- 19 kupitia wataalamu wa afya wa Jiji la Dodoma wanaotembelea ofisi yetu na watafanya zoezi hilo kwa siku tatu kuanzia leo jumanne tarehe 28 Sept 2021 hadi siku ya Alhamisi 30 Sept 2021 watakuwa wamemaliza kwa wizara yetu’’ alisema Kerra
Mkurugenzi huyo wa Utawala na Rasilimali Watu katika Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwataka watumishi wa Wizara ya Ardhi kwenye ofisi ambazo haziko kwenye Mji wa Serikali Mtumba kuwa tayari kupata chanjo hiyo kupitia ofisi zao.
Kerra alizitaja Ofisi nyingine za Wizara ya Ardhi kwa mkoa wa Dodoma ambazo haziko kwenye Mji wa Serikali Mtumba kuwa ni zile za Uhasibu zilizoko Dodoma Mjini, Upimaji, Maendeleo ya Makazi na Uthamini zilizoko Nanenane pamoja na Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani na kusisitiza watumishi wake wanatakiwa kukaa tayari kupata chanjo hiyo.
Serikali imewataka wataalamu wa sekta ya afya kuanza kuhamasisha wananchi wakiwemo watumishi wa umma kwa kuwafuata ofisni kwa ajili ya kupata chanjo ya Uviko-19 ili kujikinga na ugonjwa wa Corona ambao umechukua uhai wa watu wengi duniani.