Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Watumishi wa Umma Hakikini Taarifa Zenu – BOT
Jun 13, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Tiganya Vincent- RS Tabora

Benki Kuu ya Tanzania(BOT) imetoa wito kwa watumishi wa Umma kuharakisha uhakiki wa majina yaliyomo kwenye mifumo ya mishahara ili yaoane na  yaliyoandikwa katika Akaunti za Benki wanazochukulia fedha zao kwa ajili ya kuepuka usumbufu wakati wa malipo ya mshahara wa Julai mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Tabora na Meneja Msaidizi wa Fedha wa BOT,  Rajab Ibrahim wakati wa mafunzo ya siku moja kwa wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo juu ya utambulizi wa alama za noti na utunzaji sahihi wa noti ili kuepuka kupatiwa noti bandia na kuchakaa mapema kwa fedha hizo.

Alisema kuwa endapo mtumishi atashindwa kurekebisha taarifa zake na kuonekana kuna tofauti ya majina kati ya akaunti yake ya Benki anayopokelea mshahara na katika mifumo ya mishahara, Benki Kuu itashindwa kulimpa hadi atakapofanya marekebisho ya tofauti zilizojitokeza.

Bw. Ibrahim alisema kuwa ni vema mtumishi wa Umma akajiridhisha kuwa majina yaliyoandikwa katika hati ya malipo (salary slip) yake yako sawa na Benki yake kabla ya kumalizika kwa mwezi Juni mwaka huu ili aweze kupata mshahara wake kwa wakati.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Tabora, Afisa Tawala Mussa Khalid alisema kuwa watumishi wengi mkoani hapo wana taarifa ya zoezi hilo na wamejitokeza kufanya marekebisho ya kasoro hizo.

Alitoa wito kwa waliobaki kufanya haraka ili wasije wakapata usumbufu pindi watakapokwenda Benki kuchukua fedha na kukuta hawajaingiziwa chochote kwa sababu ya kutofanya marekebisho ya majina katika hati ya malipo na akaunti ya Benki.

 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi