Watumishi wa Umma wapatao 440 wanatarajiwa kuondoka nchini kwenda Korea Kusini kupata mafunzo ya muda mfupi ili kuongeza ujuzi katika kazi zao.
Watumishi hao ni wale wanaofanya kazi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika sekta mbalimbali ikiwamo afya, nishati, maji na nyinginezo katika ulimwengu wa leo ambapo mifumo ya kidijitali inatumika katika kutoa huduma zote kwa jamii.
Akizungumza leo jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Ndg. Mohamed Hamisi Abdulla amesema idadi hiyo ni sehemu ndogo ya watumishi wa Umma ambao wamekuwa wakisafiri kwenda nje kupata mafunzo mbalimbali tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani Machi 19, 2021.
"Leo hii inawatangazia Watumishi wa Umma uwepo wa nafasi 440 za ufadhili wa mafunzo ya muda mfupi kwenye masuala ya TEHAMA na Teknolojia zinazoibukia kwa Watumishi wa Umma.
"Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-UTUMISHI (OR-MUUUB) tutaendelea kuhakikisha tunasimamia mafunzo kwa kada hii ya TEHAMA kwa watumishi wa Umma.
"Hivyo basi napenda kuwatangazia watumishi wote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa tumefungua dirisha la maombi hayo kupitia tovuti ya www.scholarships.mawasiliano.go.tz," ameeleza Ndg. Abdulla.
Tangu alipoingia madarakani Machi 19, 2021 Rais Samia amewaruhusu watumishi wa kada mbalimbali kuondoka kwenye vituo vyao vya kazi ili kwenda kuongeza ujuzi wao kwa ajili ya maslahi ya Watanzania.