Na Mwandishi Wetu-MAELEZO,DODOMA
Serikali imesema baada ya kumaliza kufanya uhakiki wa madeni ya watumishi wa umma italipa madeni hayo katika mshahara wa mwezi februari 2018.
Akiongea na waandishi wa habari leo Mjini Dodoma Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema madai hayo yanajumuisha mishahara isiyolipwa, tofauti ya mishahara kutokana na kukaimu na nyongeza za mishahara zilizotokana na kupandishwa vyeo na kuchelewa kurekebishwa mishahara.
"Kufikia tarehe 01 Julai, 2017 Serikali ilikuwa na madai ya malimbikizo ya mishahara yenye jumla ya shilingi Bilioni 127.6 kwa watumishi 82,111 wakiwamo walimu 53,925 waliokuwa wakidai Shilingi Bilioni 53.94 sawa na asilimia 42.27 ya madai yote na wasiokuwa walimu 28186 wanaliokuwa wakidai Bilioni 73.6 sawa na asilimia 57.73" Alisisitiza Dkt. Mpango.
Akizungumzia matokeo ya uhakiki wa madeni hayo Dkt. Mpango amesema kuwa madai ya watumishi 27,389 kati ya 82,111 yenye jumla ya shilingi bilioni 43.39 ikiwa ni asilimia 34 ya madai yote ya shilingi bilioni 127.6 yaliyohakikiwa yameonekana ni sahihi na yanastahili kulipwa bila marekebisho.
Waziri Dkt. Mpango aliongeza kuwa madai yanayostahili kulipwa yanajumuisha shilingi bilioni 16.25 kwa walimu 15,919 na shilingi bilioni 27.15 kwa watumishi wasiokuwa walimu 11,470.
akifafanua kuhusu matokeo ya madai hayo yamewezesha Serikali kuokoa jumla ya shilingi bilioni 84.22 ambazo ni sawa na asilimia 66 ya madai yote ya malimbikizo ya awali ya shilingi bilioni 127.61 yaliyokuwa kwenye mfumo.
Aidha, Waziri Dkt. Mpango amesema kuwa hatua hiyo ni matokeo ya juhudi za Serikali ambazo ni pamoja na kuwaondoa kwenye mfumo wa malipo ya mishahara watumishi hewa, vyeti feki na wasio na sifa.
Serikali itaendelea kulipa madai ya watumishi kadiri yanavyojitokeza ili kuondokana na malimbikizo ya aina hii ambayo yanaweza kuisababishia Serikali hasara kwa kulipa madai yasiyostahili.