MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewataka viongozi wa mikoa, wilaya na halmashauri nchini kuhakikisha miradi inayotekelezwa kwa fedha za Serikali inasimamiwa kwa ufanisi, inakamilika kwa wakati na kwa viwango vya ubora vinavyotakiwa ili wananchi wanufaike na uwekezaji unaofanywa na Serikali.
Akizungumza Oktoba 14, 2026, wakati wa kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru mkoani Rukwa, Mhe. Ndejembi amesema usimamizi wa miradi ya maendeleo unapaswa kuwa endelevu badala ya viongozi kusubiri Mwenge wa Uhuru unapokaribia ndipo waanze kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo.

Amesisitiza kuwa fedha za umma zinapaswa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa, huku akiwataka viongozi kuwajibika katika kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa kuzingatia taratibu, ubora na thamani ya fedha ili kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya wananchi.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa kupambana na rushwa, akieleza kuwa vitendo hivyo ni kikwazo kwa haki na maendeleo kwa sababu vinachangia mikataba mibovu, ukiukwaji wa taratibu za utekelezaji wa miradi na utoaji wa huduma zisizokidhi viwango vinavyotakiwa.

Ameelekeza kuwa hatua stahiki zichukuliwe pale mapungufu, uzembe au hujuma katika matumizi ya fedha za umma zinapobainika.
Akizungumzia umuhimu wa Mwenge wa Uhuru, Mhe. Ndejembi amesema Mwenge huo ulipoasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ulikuwa na lengo la kuhamasisha wananchi kujenga Taifa huru, kufanya kazi kwa bidii na kulinda uhuru uliopatikana kwa gharama kubwa, huku ukiendeleza misingi ya haki, usawa, umoja na mshikamano.
Ameeleza kuwa Hayati Mwalimu Nyerere alitoa mchango mkubwa katika ukombozi wa Tanganyika na mapambano dhidi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi barani Afrika, pamoja na kushirikiana na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume katika kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1964.
"Misingi ya utu, haki na usawa bila kujali rangi, dini, kabila au tabaka inaendelea kuwa muhimu katika kujenga Taifa lenye mshikamano" amesema
Kuhusu mapambano dhidi ya dawa za kulevya, Makamu wa Rais amesema biashara na matumizi ya dawa hizo yanaathiri nguvu kazi ya Taifa, hususan vijana.
Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha operesheni za kuwakamata wanaojihusisha na biashara hiyo haramu, kudhibiti mashamba ya bangi na mirungi, kukamata na kuteketeza dawa za kulevya, pamoja na kuimarisha huduma za tiba na urejeshaji wa waathirika katika jamii.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), akibainisha kuwa kiwango cha maambukizi kwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi nchini ni asilimia 4.4, huku takribani watu milioni 1.5 wakiishi na VVU.
"Vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 ni miongoni mwa makundi yanayohitaji kupewa kipaumbele katika juhudi za kuzuia maambukizi mapya, kupitia elimu, upimaji na huduma za afya" amesema Makamu wa Rais

Amesema kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kinapaswa kuwa chachu ya kuongeza uwajibikaji, kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa na dawa za kulevya, pamoja na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.