Na Tiganya Vincent
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amewaagiza Walimu Wakuu wa Shule za Msingi kuhakikisha hakuna mtoto anayeanza Darasa la Kwanza bila kuwa amepitia darasa la Awali.
Hatua hiyo inalenga kuondoa tatizo la kuwa na wanafunzi wanaoingia Darasa la Kwanza bila kufahamu kusoma, kuhesabu na kuandika.
Mwanri alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akifungua mkutano wa kutathmini masuala ya elimu mkoani humo na kuhimiza walimu kuhakikisha wanaondoka tatizo la KKK shuleni kwao.
“Msingi mzuri wa mtoto lazima uanzie elimu ya awali na ndio maana nasisitiza kuwa mtoto asiingie la kwanza kama akupitia Chekechea kule ndipo mtoto anapoandaliwa kuwa na maendeleo mazuri kitaaluma hivyo ukikosea toka hapo basi mtoto anaweza kutokuwa na maendeleo mazuri darasani” alisema.
Alisema vitendo vya baadhi ya walimu kutozingatia hilo na kuchukua watoto ambao hawakupita elimu za awali ndiko kunakosababisha baadhi yao wanapofanya mitihani ya kujipama ya Darasa la Nne matokeo yao sio mazuri kwa sababu ya kuanza la kwanza hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.
Aidha, Mwanri aliwapongeza walimu wa Shule za Awali na Msingi kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuwatengenezea msingi mzuri watoto hao ili wanapoendelea na masomo yao waweze kufanya vizuri.
Katika hatua nyingine amewataka wamiliki na walimu wa Shule za Awali kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri kwa watoto hao ili wapende kwenda shule.
Alisema maeneo hayo lazima yawe na vivutio vya michezo mbalimbali ya watoto wadogo ili pamoja na kujifunza wawe na muda wa kucheza kama sehemu ya burudani na elimu kwao.
Wakati huo huo Mwanri ametoa wito kwa wazazi na wadau wengine kuweka mazingira mazuri ambayo yatawavutia walimu hasa wale ajira mpya kupenda kufanya kazi katika maeneo yao.
Alisema mazingira hayo ni pamoja na kuwawekea vivutio kama vile kuwapa maeneo ya kulima , nyumba za kuishi kama hakuna nyumba za shule na wakati mwingine kuwapa chakula cha kuanzia maisha.
Mwanri alisema kuna baadhi ya maeneo hapa nchini yamefanikiwa kielimu kutokana na wazazi kuweka vivutio ambavyo vimewafanya walimu wanaporipoti kutofikia kuhama katika shule walizopangiwa.