Na Georgina Misama – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amezitaka Taasisi zote nchini zinazoshughulikia masuala ya usajili wa wawekezaji kuacha tabia ya urasimu hasa kwa wawekezaji wa ndani kwani kuwachelewesha wawekezaji kunachelewesha nafasi za ajira kwa vijana, mapato ya kodi na kusababisha udumavu wa uchumi wa nchi.
Rais Samia alisema hayo leo Disemba 1, 2021 katika hafla ya ufunguzi wa kiwanda cha kutengenezea waya kijulikanacho kwa jina la ‘Raddy Fiber’ kilichopo Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, ambapo alisema kwamba urasimu kwa wawekezaji hauna nafasi katika Serkali ya Awamu ya Sita.
“Nchi yetu inahitaji wawekezaji kuliko sisi tunavyowahitaji, sisi tunawahitaji zaidi kuliko wao wanavyoihitaji Tanzania hatuna budi kufanya kila linalowezekana kuwavutia waje kwa wingi ili nchi yetu iweze kufaidika na uwekezaji wao. Tunapomchelewesha mwekezaji, tunachelewesha ajira, tunachelewesha kodi na tunadumaza uchumi wa nchi yetu,” alisema Rais Samia.
Aliongeza kwamba Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa ufanyaji biashara na uwekezaji ikitambua nafasi ya sekta binafsi katika mageuzi ya uchumi lengo ni kufanya kazi kwa kushirikiana na sekta binafsi ambapo alitoa mfano wa kiwanda cha Raddy Fiber kama matokeo ya Serikali kufanya maboresho katika mazingira ya uwekezaji.
“Kwa wafanyabiashara na wawekezaji wote wa Tanzania na wale wageni, baadhi yenu mpo hapa leo hii pamoja nasi, nawakaribisha sana kuwekeza na nawahakikishia usalama wa mitaji yenu pamoja na uhakika wa kuendelea kufanya biashara. Nawapongeza pia Benki ya CRDB na benki zote zilizoanza kutoa mikopo kwa wawekezaji kwa riba nafuu,” alisema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia aliwataka watendaji wa Taasisi zenye dhamana ya kutoa vibali kwa wawekezaji kuacha kasumba ya kuangalia majina ya wawekezaji na kutoa kipaumbele kwa wawekezaji kutoka nje zaidi ya wanaotoka hapa nchini na kusema kwamba hivi sasa Watanzania wamefunguka, wapo walioenda nje wakajifunza na kukusanya mitaji, wanaporudi kwa ajili ya kuwekeza wapewe nafasi na ushirikiano.
Vile vile alitoa ahadi ya Serikali ya kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ikiwemo kuboresha miundombinu muhimu kama vile maji, barabara, viwanja vya ndege, reli, mawasiliano, nishati ya umeme na gesi na kipaumbele ni kwa Mkoa wa Pwani ambao ni mkoa mteule katika uwekezaji wa viwanda.
Akiongelea umuhimu wa kiwanda hicho kwa nchi, Rais Samia alisema kwamba kiwanda hicho kimeitoa Tanzania kwenye nyanja za Kimataifa na kwamba umetafsiri kwa vitendo Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano ambapo moja ya mambo yaliyowekwa kwenye mpango huo ni uchumi wa kidigitali.
Rais Samia pia aliongelea utekelezaji wa mkongo wa Taifa ambao alisema umekamilika kwa asilimia 75 na kwamba tayari umeunganishwa na nchi nyingi zinazopakana na Tanzania zikiwemo Burundi, Rwanda, Uganda, Malawi, Zambia na Msumbiji wakati huo huo mpango wa kuunganisha na Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Congo unaendelea na utekelezaji wake utafanyika mwaka 2022-2023.
“Hii inatoa sura kama kweli Tanzania ni kitovu cha mawasiliano, tumeshakwenda nchi zinazotuzunguka na sasa tunaenda Congo, kwa jiografia aliyotujalia Mungu tumeweza kuwa kitovu cha mawasiliano lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na huduma za mawasiliano ili kufaidi fursa zinazotokana na TEHAMA.”
Kiwanda cha Raddy Fiber kilichozinduliwa leo kina uwezo wa kuzalisha kilometa 24,000 za waya kwa mwaka, kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kutoa nafasi za ajira 670 na kinatarajiwa kuwa kiwanda cha tatu Afrika na cha kwanza (1) Afrika Mashariki na Kati kwa kuzalisha bidhaa za aina hiyo.