Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Watanzania watakiwa kuuenzi Utamaduni wao kupitia JAMAFEST.
Sep 12, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_13354" align="aligncenter" width="750"] Aliyekuwa Mkurugenzi wa Masuala ya Utamaduni wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Hermas Mwansoko akitoa mada kuhusu masula ya utamaduni mbele ya Wajumbe mbalimbali waliohudhuria mkutano unaohusiana na masuala ya Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki (JAMAFEST) mjini Kampala, Uganda 12 Septemba, 2017.[/caption]

Watanzania wametakiwa kuuenzi na kuulinda utamaduni wao kupitia Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki (JAMAFEST) ili waweze kuleta maendeleo katika masuala ya ujasiriamali, utalii na pia kuufanya uwe bidhaa yao katika kuutambulisha utanzania wao hususani katika masuala ya vyakula, mavazi ya asili, nyumba za asili, utamaduni usioshikika pamoja na lugha ya Kiswahili.

Kauli hiyo imetolewa leo Mjini Kampala, Uganda na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Prof. Elisante Ole-Gabriel katika Tamasha la Kiutamaduni na Sanaa kwa nchi za Afrika Mashariki maarufu kama JAMAFEST.

Prof. Elisante ameeleza kuwa, Utamaduni ndiyo silaha pekee inayoweza kuwaweka watu pamoja ambapo amesisitiza kuwa, Watanzania hawanabudi kuulinda utamaduni wao ili uweze kuwaletea maendeleo huku akigusia suala la lugha ya Kiswahili, matumizi ya vyakula vya asili, matumizi ya mavazi ya asili pamoja na nyumba za asili kuwa vitu hivyo vina uwezo mkubwa wa kuleta maendeleo nchini.

  [caption id="attachment_13356" align="aligncenter" width="750"] Baadhi ya Washiriki wa mkutano uliohusisha utoaji mada wa baadhi ya Viongozi mbalimbali toka nchi wanachama pamoja na wageni waalikwa kuhusiana na masuala ya umuhimu wa Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki (JAMAFEST) wakisikiliza uwasilishaji mada ukioendelea mjini Kampala, Uganda leo 12 Septemba, 2017.[/caption]

Akizungumzia kuhusu matumizi ya lugha ya Kiswahili alisema kwamba, lugha hiyo imekuwa ni ya 10 kati ya lugha zinazozungumzwa Duniani na inazungumzwa na watu zaidi ya nchi 50 katika Bara la Afrika.

Ameongeza kuwa, lugha ya Kiswahili inaweza kutumika kama bidhaa ambapo juhudi za kutosha kupitia Wizara yake zinafanywa katika kuhakikisha kuwa lugha hiyo inatumika zaidi kwa ufasaha na kubidhaishwa ulimwenguni kote.

“Kupitia Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), tunahakikisha kwamba Kiswahili kinabidhaishwa ndiyo maana hivi karibuni Waziri wetu Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alizindua Kamusi Kuu ya Kiswahili Bungeni Mjini Dodoma, kwahiyo tukio lile limekuwa chachu ya pekee na limeongeza uzito mkubwa katika lugha ya Kiswahili”, alisema Prof. Elisante.

[caption id="attachment_13357" align="aligncenter" width="750"] Baadhi ya Washiriki wa mkutano uliohusisha utoaji mada wa baadhi ya Viongozi mbalimbali toka nchi wanachama pamoja na wageni waalikwa kuhusiana na masuala ya umuhimu wa Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki (JAMAFEST) wakisikiliza uwasilishaji mada ukioendelea mjini Kampala, Uganda leo 12 Septemba, 2017.[/caption]

Amebainisha kuwa, Tamasha la JAMAFEST litasaidia kuondosha tofauti mbalimbali baina ya nchi za Afrika Mashariki na litasaidia kuzifanya nchi hizo kuwa kitu kimoja kwakuwa zitakuwa zinashikamana na lugha ya Kiswahili ambayo kwa kiasi kikubwa inatumika katika nchi hizo.

“Tukiweka utamaduni wetu ukawa unaingiliana basi tutafika muda itabidi tuanze kusahihisha zaidi kufafana kwetu na sio kutofautiana kwetu na hakika hakuna atakayebaguliwa kwani umoja wetu huo utaleta faida kubwa katika masuala ya uchumi wa viwanda kwasababu soko litakuwa kubwa baina ya nchi zetu za Afrika Mashariki”, alisema Prof. Elisante.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Bibi Joyce Fissoo amesema kwamba, Tamasha la JAMAFEST limeleta fursa mbalimbali katika masuala ya utamaduni kama vile vivutio vya kiutamaduni, vivutio vya kiasili, ambapo Tanzania imepata fursa ya kuwa na mada tano zinazozungumzia masuala ya hifadhi, masuala ya filamu hususani mchango wa filamu katika uchumi wa Taifa, masuala ya filamu na muziki, masuala ya Sheria na taratibu zinazosimamia sekta za utamaduni na ubunifu.

Amefafanua kuwa, mada ambazo zimetolewa na Viongozi mbalimbali toka Tanzania zimeakisi masuala muhimu ya utamaduni, umuhimu wa kuuhifadhi utamaduni, umuhimu wa sekta za ubunifu zikiwemo na filamu.

“Tamasha la JAMAFEST linasaidia kuimarisha utangamano miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, linatanua wigo wa masoko ambapo bidhaa mbalimbali zinapatikana toka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki, pia linatangaza vivutio vya nchi wanachama, lakini pia linatangaza rasilimali za nchi wanachama ambapo kwa upande wa Tanzania tumeweka mambo ya kipekee jambo ambalo limewavutia watu mbalimbali kuja kuona vitu vyetu”, alisema Bibi Fissoo.

Katika Tamasha hilo, Tanzania imewakilishwa na wadau wapatao 247 ambapo kati yao 71 wanatoka Tanzania Visiwani (Zanzibar) ambapo baadhi ya vikundi vya ngoma na bendi vimehudhuria pia kwa upande wa Tanzania Bara kuna vikundi mbalimbali vya Sanaa toka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni (TaSUBA) pamoja na vinginevyo ambavyo vimehudhuria katika Tamasha hilo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi