Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Watanzania Watakiwa Kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa Kudumisha Muungano
Mar 25, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na washiriki katika hafla ya kuenzi maisha ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kuelekea siku yake ya kuzaliwa iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa rai kwa Watanzania kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kudumisha Muungano na kuhifadhi mazingira.

Ametoa rai hiyo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuenzi maisha ya Hayati Baba wa Taifa ambaye anatarajiwa kutimiza miaka 100 ya kuzaliwa Aprili 13, 2022.

Dkt. Jafo alisema kuwa Rais huyo wa kwanza wa Tanzania ajenda yake kubwa ilikuwa ni Muungano na Mazingira hivyo kama Watanzania tuna kila sababu ya kumuenzi kivitendo katika kumkumbuka.

Alisema kuwa takriban asilimia 40 ya ardhi hapa nchini imehifadhiwa ambapo ndani yake kuna mbuga mbalimbali za wanyama na misitu hali inayoashiria uwepo wa hifadhi ya mazingira ambayo misingi yake iliwekwa na Mwalimu Nyerere.

“Ndugu zangu tunapoadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa kama tunampenda basi tuna wajibu wa kuulinda Muungano wetu adhimu na kujali mazingira na leo hii nimefarijika kuona viongozi wa zamani wapo hapa na vijana ambao wanatamani kusikia historia ya Baba wa Taifa,” alisema.

Pia Waziri Jafo alitoa wito kwa Watanzania kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita ambayo inaendeleza mazuri yote yaliyofanywa na Serikali za awamu zilizopita ikiwemo utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutengeneza diplomasia nje ya nchi kutokana na mikutano mbalimbali aliyoshiriki na kuhutubia ukiwemo wa Mkutano wa 26 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) uliofanyika Glasgow, Scotland Novemba 2, 2021

Awali akimzunguzia Hayati Baba wa Taifa, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alisema alikuwa ni mtu mwenye upendo kwa kila mtu.

Alisema kuwa Mwalimu Nyerere alitufundisha kuwa binadamu wote ni sawa bila kujali rangi au dini hivyo na Watanzania wanapaswa kumuenzi kwa kutokuwa wabaguzi kwa namna yoyote ile. Alimtaka kila Mtanzania kutafakari amemuachia urithi gani.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wastaafu akiwemo Waziri Mkuu wa Mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba, Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Bibi Leah Lupembe pamoja na viongozi kutoka mataifa mbalimbali.

Itakumbukwa kuwa Mwalimu Nyerere alifariki dunia Oktoba 14, 1999 nchini Uingereza akiwa na umri wa miaka 77 na kuzikwa kijijini kwake Butiama mkoani Mara.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi