Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Watanzania Watakiwa Kuchangamkia Fursa Katika Sheria ya PPP
Sep 05, 2024
Watanzania Watakiwa Kuchangamkia Fursa Katika Sheria ya PPP
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Prisca Kayombo, akizungumza wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Wakuu wa Idara ya Ununuzi na Wakuu wa Idara ya Mipango kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura Na. 410, Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Sura NA. 103 na matumizi sahihi ya takwimu iliyohusisha Mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara ulioandaliwa na Wizara ya Fedha uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.
Na Josephine Majura, WF Simiyu

Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Prisca Kayombo, amewataka Watanzania kuchangamkia fursa zilizoainishwa katika Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta ya Binafsi (PPP) ili kuweza kujikwamua kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

 

Bi. Kayombo alitoa rai hiyo mkoani Simiyu, wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Wakuu wa Idara ya Ununuzi na Wakuu wa Idara ya Mipango iliyojumuisha Mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.


 

“Serikali iliona mapungufu katika Sheria ya Ubia Kati ya Serikali na Sekta ya Binafsi ndiyo maana imefanya marekebisho ambayo yanatoa fursa kwa Watanzania kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini”, alisema Bi. Kayombo.


 

Alisema kuwa marekebisho ya Sheria hiyo yanatoa fursa kwa Watanzania kufanya uwekezaji nchini ili kusaidia uchumi wa Tanzania kuimarika na kuipunguzia Serikali matumizi ya fedha za kigeni kwa kuwalipa Wawekezaji wa nje ya nchi.


 

Akizungumzia suala la matumizi sahihi ya Takwimu, alisema kuwa Serikali ya Tanzania imekuwa ikiitumia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuandaa takwimu rasmi ambazo hutumiwa na Serikali kurahisisha kupanga bajeti na mipango ya kimaendeleo kwa wananchi wake.


 

Kwa upande wake Afisa Sheria Mkuu, Idara ya Sheria, Wizara ya Fedha, Bw. Paul Kimweri alisema kuwa Serikali inaendelea kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo Watendaji mbalimbali wa Serikali katika mikoa yote nchini.


 

Aliongeza kuwa kabla ya kufanyika kwa mkutano huo, ulitanguliwa na Mkutano wa ufunguzi uliofanywa na Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ambao uliwahusisha Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na viongozi wengine wa Serikali mkoani Dodoma.


 

Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Mipango na Uratibu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga  m, Bw. Alex Mpasa, aliahidi kwenda kuzisimamia Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhakikisha  wanatekeleza Sheria  hizo kama  Sheria ilivyoelekeza.


 

Aliipongeza Wizara ya Fedha kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo Wakuu wa Idara ya Ununuzi na Mipango kwa kuwa mafunzo hayo waliyoyapata yatawasaidia kuwa na uelewa mpana wakati wa kutekeleza majukumu yao na kuwasaidia wengine ambao hawajapata mafunzo hayo.


 

Wizara ya Fedha inaendelea kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo Wakuu wa Idara ya Ununuzi na Mipango nchi nzima katika mikoa ya Kikanda ikiwemo Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati, Kanda ya Pwani, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kusini, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Magharibi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi