Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wataalam wa Afya Watakiwa Kufanya Tafiti za Kisasa
Jun 29, 2017
Na Msemaji Mkuu

 

Na: Fatma Salum 

Serikali imetoa rai kwa wataalamu wa sekta ya afya nchini kufanya tafiti nyingi za kisasa ili kuboresha huduma za afya na kuliwezesha taifa kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Rai hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Tano la Wanasayansi lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Kigwangalla alisema kuwa ili kufanikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa watu wote nchini, ni muhimu wataalamu waka kaa pamoja na kujadili namna bora ya kufanya tafiti zenye tija, ambazo zitasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya afya.

“Changamoto katika sekta ya afya ni nyingi hivyo basi wataalamu mbalimbali wa masuala ya afya wanapaswa kufanya tafiti nyingi kadri iwezekanavyo ili matokeo ya tafiti hizi yasaidie kutengeza sera na kufanya maamuzi katika masuala yanayohusu afya.” Alisema Kigwangalla.

Aidha Kigwangalla amekipongeza MUHAS kwa kuwa mstari wa mbele kwenye uandaaji wa makongamano na mikutano ya kujadili matokeo ya tafiti mbalimbali za afya na kutoa mapendekezo kwa manufaa ya jamii.

Naibu Waziri aliainisha baadhi ya maeneo yanayohitaji kujadiliwa zaidi kuwa ni pamoja na Bima ya Afya, Afya ya Mama na Mtoto na Magonjwa ya Mlipuko kama Ebola, Zika na mengineyo.

Pia aliwasisitiza MUHAS kushirikiane na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi ili kuboresha tafiti za masuala ya afya zitakazoleta teknolojia mpya ya matibabu na utoaji huduma kwa njia za kisasa ikiwemo matumizi ya mitandao ya simu kwenye kulipia huduma hizo.

Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Appolinary Kamuhabwa kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Ephata Kaaya alieleza kuwa kongamano hilo ni moja ya utekelezaji wa majukumu ya chuo hicho ambapo pia hutoa fursa na hamasa kwa watafiti wachanga kujitokeza kuleta tafiti zao ili zijadiliwe kwa manufaa ya umma.

Pia Prof. Kamuhabwa aliishukuru Serikali kwa kuendelea kukisaidia chuo hicho katika kuhakikisha kinatoa elimu bora ikiwemo kusaidia ujenzi wa kampasi yake mpya iliyopo Mloganzila itakayotumika kufundishia, kufanya tafiti na kutoa huduma za afya kwa wananchi.

Alisema kuwa kongamano hilo la siku mbili limefadhiliwa na Serikali ya Sweden kupitia taasisi ya Sida ambapo jumla ya tafiti 160 zitawasilishwa na watafiti mbalimbali wa masuala ya afya kutoka ndani na nje ya nchi watashiriki.

“Tafiti zinazofanywa na MUHAS zimejikita kwenye vipaumbele vya Taifa kwa kufuata Mkakati wa Taifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini  wa mwaka 2005, Mpango wa Taifa wa Maendeleo hadi mwaka 2025 na Malengo ya Dunia ya Maendeleo Endelevu ambapo vipaumbele hivyo ni pamoja na UKIMWI, Kifua Kikuu, Malaria, Afya ya Mama na Mtoto, magonjwa yasiyoambukiza, tafiti za mifumo ya afya, magonjwa yasiyopewa kipaumbele na tafiti za taaluma ya afya.” Alibainisha Kamuhabwa.

Kaulimbiu ya kongamano la mwaka huu ni ‘Kutumia Matokeo ya Tafiti za Afya kwa Vitendo ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu’.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi