Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wandaaji wa Michezo Watakiwa Kushirikiana na Vyama vya Mchezo
Dec 11, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Shamimu Nyaki

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul ametoa wito kwa Wadau wanaoandaa mashindano mbalimbali ya michezo kuwaalika Vyama vya Mchezo husika ili viweze kuona vipaji vinavyooneshwa katika mashindano hayo ili viweze kusaidia Taifa.

Mhe. Gekul, ametoa wito huo Desemba 10, 2022 wilayani Moshi Mjini, wakati akifunga mashindano ya michezo yaliyoandaliwa na Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi wilayani hapo ambapo amesisitiza Maafisa Utamaduni na Michezo kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Wadau wanaofanya shughuli za Utamaduni, Sanaa na Michezo katika maeneo yao.

"Jukumu la kukuza michezo sio la Serikali pekee, nawapongeza UWT kwa kuandaa mashindano haya ambayo yametoa nafasi kwa vijana kuonesha uwezo wao katika Sanaa na Michezo, naendelea kusisitiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga maeneo ya michezo, kuyalinda yasivamiwe vilevile bajeti ya michezo itumike katika michezo", amesisitiza Mhe. Gekul.

Aidha, ameitaka Jamii kuzingatia maadili, mila na desturi  za Tanzania zilizo njema na kujiepusha na vitendo vya Ukatili wa kijinsia, huku akieleza kuwa upatikanaji wa Vazi la Taifa, Kamati iliyoundwa na Waziri Mhe. Mohamed Mchengerwa inaendelea na kazi hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT wilayani hapo, Mhe. Theresia Komba amesema lengo la mashindano hayo ni kuimarisha afya, kujenga uhusiano miongoni mwa jamii, kuinua vipaji pamoja na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

Mashindano hayo yamehusisha mpira wa miguu wanawake, Netiboli, kuvuta kamba pamoja na michezo ya jadi ikiwemo kukimbia na magunia, kufukuza kuku, huku  yakipambwa na burudani kutoka kwa Wasanii wa wilaya hiyo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi