Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Serikali na sekta binafsi kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa wanawake wanashiriki kikamilifu katika fursa za uchumi wa kidijitali ili waweze kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.
“Viongozi wa Serikali, sekta binafsi, wadau wa maendeleo, wananchi wekeni mikakati ya pamoja ya kukuza ushirikiano na kuwekeza kwenye miundombinu ya TEHAMA ili kutoa kipaumbele katika kuongeza ujumuishi wa kidijitali na wa kifedha.”
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Februari 15, 2024) alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua mkutano wa Future Ready Summit katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Katika mkutano huo ulioandaliwa na kampuni ya Vodacom, Waziri Mkuu ametoa wito kwa makampuni ya simu yaweke gharama rafiki za mawasiliano ili kuvutia washiriki wengi wakiwemo wanawake kushiriki katika fursa za uchumi wa kidijitali.
Pia, Waziri Mkuu amewataka wadau wa sekta binafsi, watumie majukwaa kama hilo la Future Ready Summit pamoja na kuandaa programu za kuwawezesha vijana, hususan wakike ili nao waweze kushiriki katika kuchangia uchumi wa Taifa.
“Kwenu washiriki wa mafunzo tumieni fursa hii vema, shirikianeni na wawezeshaji, muwe na mijadala yenye tija ili mafunzo yawe na tija inayotarajiwa. Aidha, mkawe mabalozi wazuri kwa wasichana na wanawake kuhusu fursa zakidijitali na matumizi ya TEHAMA.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali inatekeleza mradi wa ujenzi wa shule za sekondari 26 za kitaifa za wasichana mahsusi kwa masomo ya sayansi ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwachochea wanafunzi wa kike wapende masomo hayo.
Mheshimiwa Majaliwa amesema shule hizo zinajengwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara kwa gharama ya shilingi bilioni 104 ambapo ujenzi wa kila shule moja inagharimu kiasi cha shilingi bilioni nne.
“Katika hili ninampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa kuhamasisha masuala ya sayansi, teknolojia na hisabati. Hii ni kutokana na utashi wake na hatua za makusudi alizozichukua kuhakikisha wasichana wanashiriki kikamilifu katika fursa za masomo ya sayansi na hisabati.”
Awali, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alitumia fursa hiyo kuwaondoa hofu Watanzania juu ya mapinduzi ya teknolojia na kuwataka wajipange na wasonge mbele.
Pia, Waziri huyo alisema jukumu la wizara hiyo ni kuhakikisha kuwa uwekezaji unafanyika kwenye ujenzi wa miundombinu ya taasisi na vyuo ambavyo vitafundisha masomo hayo. Alisisitiza kuwa Tanzania ipo tayari kwenda mbele katika Mapinduzi ya kiteknolojia.