Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wanawake Waipongeza Serikali Kuboresha Huduma za Afya, Elimu
Mar 08, 2025
Wanawake Waipongeza Serikali Kuboresha Huduma za Afya, Elimu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia Wananchi kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha tarehe 08 Machi, 2025.
Na Grace Semfuko, MAELEZO

Tanzania imeungana na mataifa mbalimbali ulimwenguni kudhimisha Siku ya Kimataifa ya  Wanawake ambapo wanawake wa Tanzania wameshiriki maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa jijini Arusha leo Machi 8, 2025 kwa kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuboresha huduma za afya, hasa afya ya Mama na Mtoto.

Wanawake hao wamesema hatua ya uboreshaji wa sekta ya afya imesaidia kuimarisha ustawi wa afya zao. Mmoja wa wanawake hao, Juliana Mollel mkazi wa Arusha mjini amesema hali imebadilika na kuelezea kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kuboresha sekta ya afya na ile ya elimu.

"Tunaishukuru Serikali kwa kuimarisha huduma za afya za mama na mtoto, siku hizi hata ukienda hospitali za chini kabisa unakuta kuna vifaa vyote muhimu vya kumfanya mama ajifungue salama na pia vinafanya upasuaji".

Kwa upande wa wanawake wa jamii za wafugaji, hali inaonekana kubadilika kwa kiasi kikubwa,  ambapo wamesema kuwa tofauti na miaka ya nyuma, sasa wanapata elimu na fursa zaidi, ikiwa ni matokeo ya ujenzi wa shule vijijini na juhudi za kuhakikisha watoto wa kike na wa kiume wanapata haki sawa ya elimu.

Anita Saitoti, mkazi wa Arusha ambaye pia mmoja wa wanawake wa kabila la wamaasai, amesema kwa sasa jamii hiyo inatapa elimu ambapo wanawake wa jamii hiyo wamekuwa wakifanya vizuri kwenye ajira.

"Kwa sasa jamii yetu inaendelea, tunapata elimu, mimi mwenyewe nimesomeshwa na sasa niko kijijini ninafundisha wanafunzi wakiwepo wamaasai wenzangu, kwa ujumla wanawake wameanza kuonekana katika kila idara na kwa sasa kuna Wakurugenzi, Walimu, Wakuu wa Wilaya, na hata Wakuu wa Mikoa ambao ni wamaasai," amesema Bi. Saitoti.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi