Na Tiganya Vincent - RS Tabora
Mfuko wa Taifa Bima ya Afya (NHIF) umewataka wanachama wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) kujinga Bima ya Ushirika Afya kwa ajili ya kuwawekea mazingira mazuri ya kuwapatia matibabu mwaka mzima.
Kauli hiyo imetolewa jana (leo) mjini Tabora na Afisa Matekelezo Mwandamizi wa NHIF, Salvatory Okumu kwenye mkutano Mkuu wa 25 wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU).
Alisema mkulima atakayejiunga na Ushirika Afya kupitia Chama chake cha Msingi (AMCOS) atakuwa na faida ya kupata matibabu kuanzia katika Zahanati hadi kwenye Hospitali za Rufaa kwa gharama nafuu ikilinganisha na kulipa fedha taslimu.
Okumu aliongeza kuwa mwanachama wa chama cha msingi cha ushirika atatakiwa kulipa shilingi 76,800/- na akitaka kulipia mtoto atatakakiwa naye amlipie shilingi 50,400/- aweze kupata matibabu mwaka mzima.
Alisema bima imeona kuwa mwanaushirika anakuwa na uhakika wa matibabu kipindi cha mavuno na baada ya hapo anapokuwa ameshauza mazao yake na kumaliza fedha anapata wakati mgumu kupata matibabu.
Okumu alisema bima ya Afya inavyo vituo 7000 nchi nzima vinavyotoa huduma ya matibabu ambapo kama mwanaushirika atajiunga chini ya Mpango wa Ushirika Afya naye atapata huduma.
Aliongeza kuwa mkulima uwa na msimu mmoja katika mwaka mmoja na unapokwisha hungojea mwaka mwingine ndio apate fedha jambo ambalo linawafanya wauze mali zao kama vile mashamba ili kupatiwa matibabu.
Okumu alisema kuwa fedha wanayotakiwa kuchangia ni kidogo ukilinganisha na gharama halisi za huduma ambazo atanufaika nazo kwa mwaka na kuongeza kuwa kuna vipimo vingine vinagharimu zaidi ya 300,000/- na dawa na matibabu ya baadhi ya magonjwa inafika hadi milioni 6,000,00O/- lakini mkulima kupitia Ushirika akichangia 76,800 atanufaika mwaka mzima.