Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wanao Wanyanyasa Watoto Kijinsia Wachukuliwe Hatua
Jun 19, 2017
Na Msemaji Mkuu

Ben Komba.

Mwishoni mwa wiki hii Mkoa wa Pwani uliungana na mikoa mingine kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika ambayo ilifanyika katika Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo.

Awali akizungumza katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika mwakilishi kutoka Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA) Bi. Penzi Nyamingumi amesema siku hiyo ni maalum kwa kuwakumbuka wanafunzi waliouawa Sharpville Soweto nchini Afrika kusini wakati wakidai haki ya elimu.

Bi.  Nyamingumi ameongeza kuwa wanafunzi hao walikuwa wanadai haki sawa wakitaka mitaala yao ifanane na mitaala ya wanafunzi weupe, ambapo kwa hapa kwetu serikali imejitahidi kwa kuanzisha programu mbalimbali kama MMEM, MMES na sasa kufikia hatua ya kutoa elimu bure kwa lengo la kumpatia mtoto haki ya elimu.

Akisoma taarifa ya watoto, Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Chalinze Bw. Frank Makala amesema Halmashauri hiyo imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha vituo vyote  kumi na saba vya malezi ya watoto  ambapo vituo kumi na nne vinamilikiwa na taasisi binafsi na vitatu vinavyomilikiwa na taasisi za dini vinatoa huduma kwa kiwango stahili.

Mgeni rasmi katika shughuli hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze, Bw. Hamis Zikatimu amewataka wenye mamlaka katika kutoa haki kwa watoto kusimamia jambo hilo ili kuimarisha utoaji wa haki za watoto kwa kuhakikisha wanaohusika na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia wanachukuliwa hatua.

Nae,  Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Mkoani Pwani, Bi. Mwamvua Mwinyi amewataka waandishi kutumia kalamu zao katika kung’amua na kuweka wazi vitendo vya unyanyasaji wa watoto.

Mwisho..

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi