Na Mwandishi Wetu
Wananchi wameshauriwa kuzingatia matumizi sahihi ya marumaru (tiles) wakati wa ujenzi ili kuepukana na madhara makubwa yatakayojitokeza.
Hayo yamesemwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Mhandisi wa Ujenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mhandisi Innocent Johnbosco wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake.
Mhandisi Innocent amesema madhara ya kutumia marumaru ambazo si sahihi au mahala si sahihi inaweza kuleta madhara kama kuteleza na kusababisha madhara makubwa kimwili.
"Wengine wanaweza wakawa wanazalisha wanatumia madini ambayo yameshakatazwa na bahati nzuri hatuna hizo kesi hapa kwetu lakini kuna wengine wanaweza kuchanganya baadhi ya madini ambayo yana madhara kwa binadamu". Amesema Mhandisi Innocent.
Amesema kwa mujibu wa viwango, kuna kiwango cha marumaru namba 954 ambacho kinazungumzia ubora na namna gani unaweza kufikia ubora wa marumaru za sakafuni na ukutani.
Aidha, Mhandisi Innocent amesema kuwa kupitia viwango namba 954 cha mwaka 2018, viwango vinagawanyika kutegemea na namna ya uzalishaji, namna marumaru hizo zinavyonyonya maji pamoja na uwezo wa kuhimili kiasi gani cha michubuko.
"Katika kiwango hicho namba 954 kimefafanua namna gani ya kufikia ubora hasa kwa wazalishaji wetu wa ndani ili waweze kuzalisha vigae ambavyo vinakidhi matakwa ya soko lakini inakidhi malengo yaliyokusudiwa kwa ajili ya matumizi". Amesema Mhandisi Innocent.
Pamoja na hayo, Mhandisi Innocent amesema ili kuweza kujiridhisha na ubora wa marumaru, kwenye kifungashio cha marumaru kwa wale wazalishaji wa ndani wanatakiwa kufuata matakwa ya kiwango hasa kutaja kiwango ambacho kimetumika katika uzalishaji wa marumaru pia waandike aina ya marumaru iliyopo humo ndani kwa maana kuna aina nyingi ambazo zinatumika katika matumizi mbalimbali.