Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Switbert Mkama amewataka wanufaika wa mradi wa kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) kuutunza ili iwanufaishe.
Ametoa rai hiyo alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua shughuli mbalimbali za mradi huo zinazofanyika katika vijiji katika Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.
Akizungumza na wanachama wa kiwanda kidogo cha kutengeneza bidhaa za ngozi katika Kijiji cha Jitegemee, Dkt. Mkama amewapongeza kwa kuendeleza ushirikiano katika kuendesha shughuli zao.
“Tumeridhika na maendeleo yenu, huu mradi ni wa kwenu sio wa Serikali kwa hiyo nawaomba muutunze mradi huu kwa ajili yenu na pia uwe darasa kwa wengine ili nao waige mfano wenu, kwani ninyi mkifanya vizuri na wengine wataiga na hivyo mtakuza uchumi wa wananchi wa hapa,” alisema.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo aliwashauri kuhifadhi benki na kutumia vizuri fedha zinazotokana na mauzo ya bidhaa zao za ngozi wanazozalisha ili ziwasaidie kupata maendeleo.
Kutokana na changamoto ya ukosefu wa mashine kwa ajili ya shughuli zao, Dkt. Mkama alisikia kilio chao na kuahidi Serikali kutatua kwa kuwapelekea vitendea kazi hivyo ambapo alimuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro kusimamia zoezi hilo.
Kutokana na changamoto hiyo aliielekeza halmashauri hiyo kurahisisha michakato ya ndani ya manunuzi ili kutowakwamisha wananchi wanaofanya shughuli hizi chini ya mradi huo.
Wakizungumza mbele ya kiongozi huyo wakati wa ziara hiyo, baadhi ya wananchi wanufaika wa Mradi wa EBARR waliishukuru na kuipongeza Serikali kwa kuwajali katika changamoto ya mabadiliko ya tabianchi inayowakabili.
Bi. Zaina Shekilango ambaye ni mwenyekiti wa kikundi kinachojihusisha na uzalishaji wa bidhaa za ngozi alimshukuru Naibu Katibu Mkuu kwa nasaha alizowapatia kuhusu uendeshaji wa kikundi kwa tija.
Aliomba viongozi waendelee kuvitembelea vikundi vyao ili waendelee kupata elimu kuhusu namna bora ya kusimamia mradi wao kwani bado wanaendelea kujifunza.
Mbali na kiwanda hicho kidogo pia katika ziara hiyo, Dkt. Mkama alitembelea na kukagua shughuli mbalimbali zikiwemo josho la mifugo na birika la kunyweshea mifugo, uchimbaji wa lambo jipya pamoja na ufugaji wa mbuzi 50 katika Kijiji cha Irkujit.
Maeneo mengine aliyotembelea ni mabanda mawili ya kuku wa mfano na kuku 850 kwa vikundi vya ufugaji wa kuku katika vijiji vya Jitegemee na Mkumbi.
Dkt. Mkama yupo katika ziara ya kutembelea na kukagua shughuli zinazotekelezwa kupitia Mradi wa EBARR chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais katika wilaya mbalimbali.