Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wananchi Washukuru Kujengewa Shule Mpya ya Nyombo
Jan 10, 2024
Wananchi Washukuru Kujengewa Shule Mpya ya Nyombo
Muonekano wa shule mpya ya Sekondari ya Nyombo iliyojengwa na Serikali katika Halmashauri ya Njombe mkoani Njombe
Na Jacquiline Mrisho - Maelezo

Wananchi na wazazi wa Kata ya Ikuna iliyopo katika Halmashauri ya Njombe wameishukuru Serikali kwa kuwajengea shule mpya ya Sekondari ya Nyombo kwani imekuwa mkombozi kwa watoto wanaokaa mbali na Shule ya Sekondari Ikuna ambayo ndiyo inayotegemewa na wakazi wa maeneo hayo.

Wananchi hao wameonesha furaha yao walipokuwa wakizungumza na Maafisa kutoka Idara ya Habari - Maelezo waliofika katika Kata hiyo kujionea maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya Serikali inayoendelea kutekelezwa mkoani Njombe.

Mwananchi wa Kata ya Ikuna, Vumilia Mlowe ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuleta mradi wa shule kwani kutokana na changamoto mbalimbali zilizokuwepo, ilikuwa ngumu wanafunzi kufaulu masomo yao hasa kwa watoto wa kike ambao wengi wameshindwa kufikia malengo kufuatana na hali halisi ya mazingira yaliyowafanya wengine kupata mimba na kulazimika kuacha shule.

"Mradi huu umetusaidia hata sisi wazazi kuweza kutekeleza mahitaji ya watoto ambayo tulikuwa tukishindwa kuyatekeleza zamani kutokana na umbali wa shule, ukaribu wa shule uliopo sasa, tunaamini mahitaji mengine yatapungua," alisema Bi. Vumilia.

Kwa upande mwingine, ameipongeza Serikali kwani kupitia mradi huo kumejengwa jengo la TEHAMA litakalowasaidia wanafunzi kupata elimu itakayoendana na ulimwengu wa sasa kwa kuwa mambo mengi yanafanyika kwa kutegemea TEHAMA.

Naye mwananchi Devis Mlawa ameshukuru kwa kupata shule yenye viwango vya juu vya ujenzi wa miundombinu inayotakiwa ikiwemo maabara bora ambazo zitawafanya wanafunzi waweze kusoma kwa vitendo na kuongeza maarifa zaidi.

Mwananchi Epson Kiyao ameeleza kuwa shule hiyo imekuja kwa muda muafaka kwani wanafunzi walikuwa wanatembea umbali mrefu kwenda kufuata shule ambapo kwa sasa watoto wataweza kufika shule kwa wakati na bila kuchoka, pia watasoma kwa bidii kutokana na mazingira bora yaliyopo katika shule hiyo mpya.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Ikuna ambaye pia ni Msimamizi wa Ujenzi wa Shule ya Sekondari Nyombo, Hussein Chaula amesema kuwa Serikali ilipeleka shilingi milioni 583.2 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari Nyombo ambapo uwepo wa mradi huo unaleta tija kwa Kata ya Ikuna kwa sababu idadi ya wanafunzi waliokuwa wanachaguliwa kwenda Shule ya Sekondari Ikuna ilikuwa kubwa, hivyo ujenzi wa shule mpya utapunguza wingi wa wanafunzi waliokuwa wakisoma Shule ya Sekondari Ikuna.

“Fedha hizo zimetumika kujenga madarasa 8, ofisi za Walimu, jengo la TEHAMA, maktaba, maabara ya fizikia, kemia na baiolojia, kichomea taka, vyoo, kinara cha maji. Mradi  huu umefikia hatua za umaliziaji na tunatarajia shule itaanza rasmi kutoa elimu Januari, 2024 kwa kupokea wanafunzi zaidi ya 200," alimalizia Mwalimu Chaula.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi