Wananchi mkoani Rukwa wameaswa kuendelea kuitunza amani katika kipindi chote cha kampeni wakati nchi ikielekea kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika siku ya Jumatano tarehe 28.10.2020 utakaowapa nafasi ya kuwachagua Madiwani katika ngazi za Kata, Wabunge katika ngazi za Majimbo pamoja na kumchagua Rais wa nchi ya Tanzania.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mh. Joachim Wangabo alipotembelea baadhi ya vijiji wilayani Nkasi ili kuhamasisha utulivu na kuasa wananchi kutovunja udugu kwa sababu za kisiasa hali itakayowapelekea kushindwa kushirikiana na kufanya maendeleo katika vijiji vyao hasa baada ya kuisha kwa uchaguzi huo na washindi kupatikana.
Aidha, amewataka wanaoshiriki katika kampeni hizo kutotumia lugha za matusi na kutanguliza kuheshimiana bila ya kusahau kuwa kinachowaunganisha ni udugu uliopo baina yao na hivyo wasijisahau wakatawaliwa na maneno yasiyo na ustaarabu na zaidi kutokubali kuvurugwa na kauli za wanaojinadi na wanaohamasisha vurugu katika kampeni zao.
“Niwaombe ndugu zangu wakati wa kampeni, huyu anaweza akawa yupo CHADEMA, huyu NCCR – Mageuzi, yule wa Chama cha Mapinduzi, lakini sisi sote si ndugu, kwa nini mpigane ngumi kwa sababu ya uchaguzi, kwanini mtoane ngeu wakati wa uchaguzi, uchaguzi unakwisha, mwezi Novemba Rais anasimikwa pale anaapishwa, ninyi si tutaendelea kuwa ndugu? Sasa kwanini muuane kwa sababu hiyo?” Alihoji.
“Watu wakija na kampeni zao wakifanya mbwembwe, wakihamasisha kupigana, mkatae mambo ya fujo kwa sababu ninyi mnaishi pamoja ni ndugu, hayo mambo yatapita mpaka tena baada ya miaka mitano, kwa hiyo mimi natahadharisha kwamba kipindi cha kampeni, kampeni zifanyike za kistaarabu, lakini watu waheshimiane, kusiwe matusi tukijua kwamba sisi ni ndugu,”Alisema.
Kampeni za Uchaguzi wa Mwaka huu zinatarajiwa kuanza tarehe 26.8.2020 huku wabunge mbalimbali wakiendelea kuchukua na kurudisha fomu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutoka kwa wasimamizi wa majimbo katika halmashauri mbalimbali.