Na Genofeva Matemu – Chato, Geita
Wananchi wa Mkoa wa Geita na mikoa ya jirani wametakiwa kufuata huduma za matibabu hospitali pindi wanapojisikia kuumwa ili waweze kupata tiba halisi na kuondoa fikra potofu za kufuata tiba hisia zinazotolewa na watu ambao sio wataalam wa afya.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mhe. Martha Mkupasi wakati wa uzinduzi wa kambi maalum ya matibabu ya moyo ya siku tano inayofanywa na wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) inayoendelea katika Hospitali hiyo.
Mhe. Martha alisema kuwa lengo la Serikali ni kusogeza huduma karibu zaidi kwa wananchi pamoja na kuwapunguzia gharama za kufuata huduma za matibabu mbali ya makazi yao ndio maana leo hii Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato inajengewa uwezo ili nayo iwe sehemu ya kusogeza huduma na kupunguza gharama kwa wananchi wa Mkoa wa Geita.
“Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato imewekezwa vifaa vyote vya matibabu ya moyo vyenye gharama kubwa hivyo nawaomba wananchi wote mtakaposikia dalili za kuumwa mfike katika Hospitali hii ili muweze kupata tiba halisi muache kwenda kwenye tiba hisia”, alisema Mhe. Martha
Mhe. Martha alisema kuwa ujenzi wa CZRH ulianza awamu ya tano ambapo Mhe. Rais wa awamu ya sita mama Samia Suluhu Hassan aliahidi kuhakikisha miradi yote iliyoanza awamu ya tano inakamilika na inafanya kazi kwa asilimia 100 jambo ambalo linathibitishwa leo katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya Kanda Chato.
“Nawaomba wataalam wa afya wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato kuweka jitihada ya pekee kupokea yale wanayofundishwa na wataalam wa afya kutoka JKCI ili baada ya kambi hii muweze kuwahudumia na kuwapatia matibabu wananchi wa Chato, mikoa ya jirani pamoja na nchi zilizopo jirani na Chato”,
“Nawashukuru watumishi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo ambao hawakuona umbali wa Wilaya yetu ilipo bali wao walidhamiria kuja kutoa huduma za matibabu ya moyo na kuleta faraja kwetu sisi wananchi wa kanda ya ziwa”, alisema Mhe. Martha.
Akizungumzia kambi hiyo ya uchunguzi na matibabu ya moyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, Prof. William Mahalu alisema kuwa wataalam wa afya wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato wamekua na utayari wa kupokea ujuzi unaotolewa na watalaam wa JKCI kwa kuwa mstari wa mbele kufanya kazi kwa pamoja na wataalam hao jambo ambalo linatoa motisha ya kuendelea kuwajengea uwezo.
Prof. Mahalu alisema kuwa jitihada zinazofanywa na wataalam wa afya wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato kama zitaendelezwa kwa kujengewa uwezo mara kwa mara na kupelekwa masomoni kwa ajili ya kuwa wataalam wabobezi wa magonjwa ya moyo kutaifanya hospitali hiyo kuwa hospitali bingwa ya magonjwa moyo nchini na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu
“Nilivyoteuliwa na Rais wa Awamu ya Tano kuwa Mwenyekiti wa Bodi hii ya JKCI nilipewa agizo la kupunguza idadi ya wananchi wanaokwenda nje ya nchi kutibiwa moyo ambapo hadi sasa tumebakiza asilimia nne tu ya wagonjwa wa moyo wanaokwenda nje ya nchi kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya moyo, asilimia hii nne tunaweza kuifuta kabisa kama wataalam wa CZRH mtajitoa kuifanya hospitali hii kuwa hospitali bingwa ya magonjwa ya moyo”, alisema Prof. Mahalu
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kuwa JKCI imejipanga kuwafuata wananchi walipo ambapo kwa kuanza JKCI itaanzisha vituo viwili vya kuchunguza magonjwa ya moyo kwa lengo la kusogeza huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wananchi.
“Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato ni moja ya kituo cha uchunguzi na matibabu ya moyo ambapo leo hii tumezindua kliniki ya matibabu ya moyo lakini pia Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mtwara nayo itakua kituo kingine cha kuhudumia wagonjwa wa moyo”
“Tumekuwa tukifanya kambi maalum za matibabu (outreach) katika Mkoa wa Dar es Salaam na kuwafanya wananchi wa mikoa mingine kusafiri kufuata huduma hizo, lakini sasa tumeona nimuhimu kuwafuata wananchi walipo ili pia tuweze kutoa mafuzo kwa wataalam wa afya tutakaowakuta sehemu tunazopeleka huduma hizi”
Aidha, Dkt. Kisenge alisema kuwa Kituo cha uchunguzi na matibabu ya moyo cha Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato kitakapoimarika kitakua kikitoa huduma za upasuaji mkubwa wa moyo na kuwekeza mtambo wa Cathlab ambao utatumika kutoa huduma za upasuaji wa moyo wa tundu dogo.
“Tunakwenda kutengeneza mpango mkakati wa kuhakikisha katika miaka mitano huduma za upasuaji wa moyo na matibabu kwa kutumia mtambo wa Cathlab zinafanyika hapa Chato ikiwa ni njia ya kuwasaidia wananchi wa Kanda ya Ziwa na nchi za jirani”, alisema Dkt. Kisenge
Naye mwananchi wa Chato aliyepatiwa huduma wakati wa kambi hiyo, Omary Maulid alisema kuwa hakuwahi kujua kama ana tatizo la shinikizo la damu na kisukari kwani mara zote alizokua akienda hospitali na kumweleza daktari kuwa macho hayaoni vizuri hakupimwa shinikizo la damu wala sukari hivyo kujikuta anatibiwa vitu vingine.
“Nimefurahi kupata fursa hii ya kuja kuchunguza afya ya moyo wangu kwa sababu nimekua nikiumwa siku nyingi, macho yangu hayaoni vizuri kumbe nina shinikizo la juu la damu ambalo sikuwahi kupimwa leo hii ndio nimejitambua”,
“Elimu ya afya hasa hii ya magonjwa yasiyoambukiza inatakiwa kutolewa zaidi sio tu kwa wananchi lakini pia na kwa wataalam wa afya waliopo katika vituo vya afya katika jamii zetu ili wananchi tuweze kupata tiba sahihi pale tunapoumwa”, alimalizia Omary