Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wananchi Mtego wa Simba wafurahia kuwashiwa Umeme
Jul 12, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Veronica Simba – Morogoro

Wananchi wa Kijiji cha Mtego wa Simba, Kata ya Mikese, Wilaya ya Morogoro Vijijini, wameshindwa kuzuia furaha yao baada ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, kuzindua rasmi uwashaji wa umeme katika Kijiji hicho, kupitia Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (REA IIIA.)

Tukio hilo la kuwasha umeme lilifanyika leo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mjini, Regina Chonjo ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Omari Mgumba, Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, ambao muda wote walionesha bashasha, Mgumba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo, aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Nishati, kwa kuendelea kutekeleza ahadi ya kuwapelekea wananchi, hususan walioko vijijini nishati ya umeme.

“Serikali iliahidi kwamba itasambaza umeme kwa vijiji vyote vilivyobaki, kwenye Awamu mbili za REA III. Tunatoa shukrani sana kwa kuja hapa leo kutekeleza ahadi hiyo kwa vitendo.”

Akizungumza katika Hafla hiyo, Naibu Waziri aliwaeleza wananchi kuwa baada ya uzinduzi huo, wataanza kuunganishiwa umeme katika nyumba zao kuanzia Ijumaa, Julai 13, mwaka huu.

“Nimeongea na Mkandarasi, kuanzia Ijumaa, zile nyumba za awali 62 zote zitawekewa umeme.”

Mbali ya uzinduzi huo wa uwashaji umeme, Naibu Waziri alitembelea Zahanati iliyopo katika Kijiji cha Towero, Kata ya Mlimani, Wilaya ya Morogoro Mjini, kwa lengo la kujionea hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa agizo alilolitoa kwa Uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Machi 24 mwaka huu, kuiunganishia Zahanati hiyo umeme.

Naibu Waziri alikiri kufurahishwa na Uongozi wa TANESCO kwa kutekeleza agizo hilo kwa wakati, ambapo mbali na kuiunganishia zahanati husika umeme, wameunganisha pia huduma hiyo muhimu kwa Shule ya Msingi iliyopo eneo hilo na kueleza kuwa wana mpango wa kupeleka umeme huo kwa Shule ya Sekondari ya mahala hapo.

“Kipekee niwapongeze TANESCO Mkoa na Makao Makuu kwa kuendelea kutekeleza maagizo ya viongozi wetu ya kupeleka miundombinu ya umeme kwenye huduma za kijamii ikiwemo zahanati, vituo vya afya, shule mbalimbali, miradi ya maji na nyinginezo.”

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo kwa Naibu Waziri, Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Lawrance Maro, alisema kuwa Transfoma iliyofungwa ili kuwezesha kuunganisha umeme huo ni yenye uwezo wa  kilovoti 50 na kwamba wamejenga njia ndogo ya kusafirisha umeme, yenye urefu wa kilomita 1.5.

Aidha, Naibu Waziri alitembelea Mtaa wa Mafisa, Kata ya Tungi, Wilaya ya Morogoro Mjini, ambapo aliridhishwa na hatua iliyofikiwa katika kutekeleza agizo alilolitoa Machi 24 mwaka huu, kuanza kazi ya kupeleka umeme katika eneo hilo.

“Namshukuru Mungu kazi imeanza na inaonekana. Tumeona njia ya umeme imeanza kujengwa na nguzo zimeanza kuchimbiwa. Kazi hii kwa awamu ya kwanza itagharimu shilingi milioni 107,” alisema.

Naibu Waziri Mgalu yuko katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme katika mikoa kadhaa nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi