Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, Septemba 26, 2023 anatarajia kuwasha umeme unaosambazwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika Kijiji cha Ihako kilichopo wilayani Bukombe, mkoani Geita.
Wananchi wa kijiji hicho wameeleza namna watakavyotumia fursa ya kufika kwa umeme wa REA kijijini hapo na kuwaongezea kipato chao cha kila siku.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutuletea umeme wa REA katika kijiji chetu, ni muda mrefu tulikuwa na changamoto ya kukosa umeme hapa kijijini; Ilikuwa inatulazimu kufuata baadhi ya huduma katika vijiji vya karibu vyenye huduma ya umeme, kama vile kukoboa na kusaga nafaka,” amesema Veradiana Renard Mkazi wa Kijiji cha Ihako.
Ameendelea kusema kuwa, atatumia fursa ya kuwashwa kwa umeme wa REA kijijini hapo kwa kufungua saluni ya kike ili kuongeza kipato chake, ambapo kwa sasa anajishughulisha na biashara ya genge.
Kwa upande wake, Nyanda Mperwa ambaye ni mkazi wa kijiji hicho, amesema kwa sasa anajishughulisha na huduma ya kuchaji simu kwa kutumia sola, lakini kutokana na ujio wa umeme kijijini hapo, amejipanga kutanua biashara yake kwa kuuza vinywaji baridi na kuweka miziki kwenye simu, huduma ambayo haikuwepo kijijini hapo kutokana na kutokuwepo kwa umeme.
“Ujio wa umeme wa REA utaibua biashara nyingi hapa kijijini, mfano huduma ya mashine ya kukoboa na kusaga nafaka, huduma ambayo tulikuwa tukiipata kwa kutembea umbali mrefu, lakini kwa sasa huduma hii itapatikana hapa kijijini kutokana na uwepo wa umeme wa REA,” amesema Sophia Yohana mkazi wa Kijiji cha Ihako.
Aidha wananchi hao wameeleza, walikuwa wakipata changamoto ya giza katika kijiji chao, lakini kutoka na uwepo wa umeme wa REA ulinzi utaongezeka kijijini hapo, pia itawapa urahisi wa kuona wanyama hatarishi katika maeneo yao kama nyoka na fisi.
“Tunamshuru Rais Samia kwa kutuletea umeme wa REA, tulikuwa na changamoto kubwa ya giza hapa kijijini, ambapo tulilazimika kuingia majumbani mapema kuogopa wanyama wakali kama nyoka na fis; Kuwashwa kwa umeme wa REA kutatuwezesha kuwaona kwa urahisi wanyama wa kali, hivyo kupambana nao kwa urahisi, tofauti na unapokutana nao kwenye giza,” amesema Peleka Shimoga, mkazi wa kijijini hapo.