Na Mwandishi Maalum – JKCI
Jumla ya watu 62 wamefanywa vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echo Cardiogram) na umeme wa moyo (ECG) wakati wa punguzo la gharama za matibabu kwa wagonjwa wa kulipia lililotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Punguzo hilo lilitolewa hivi karibuni na Taasisi hiyo ikiwa ni sehemu ya kusherehekea ushindi wa timu ya Taifa ya mpira wa miguu kwa kuifunga timu ya Uganda mabao 3-0 na kuweza kushiriki katika mashindano ya Taifa Bingwa Barani Afrika AFCON. 2019.
Akiongea na mwandishi wa habari hizi jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tiba Shirikishi ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo Dkt. Delila Kimambo alisema kati ya wagonjwa 62 waliopima afya zao nane walikuwa ni watoto.
Dkt. Delila alisema katika kusherehekea ushindi wa timu ya Taifa Taasisi hiyo imeona ni vyema kufungua milango na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kupima afya ya moyo.
“Kati ya watu 62 tuliowapima 19 tuliwakuta na matatizo ya moyo ambapo wa nne wanatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa mishipa ya damu ya moyo, mmoja kati yao ameshafanyiwa na kukutwa na tatizo la kuziba kwa mishipa miwili ya damu ameshazibuliwa mshipa mmoja na anaendelea vizuri”,.
“Wengine wanne walikutwa na tatizo la valvu ambapo wawili wanatakiwa kufanyiwa upasuaji wa kubadilisha valve. Wengine tumewakuta na shinikizo la juu la damu”,.
“Zoezi hili limefanyika vizuri, tunafahamu kuwa kuna wananchi ambao huwa wanahitaji vipimo vya moyo kwa dharula na hawawezi kufika kwetu kutokana na shida mbalimbali za maisha, hivyo tulitoa punguzo hili la bei ili kuwafungulia milango ya kupata matibabu ya vipimo vinavyoweza kugundua kama mtu ana magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Delila.
Dkt. Delila alimalizia kwa kuwaomba watanzania kuwa na utamaduni wa kupenda kupima afya zao mara kwa mara ,kupata matibabu na majibu ya magonjwa yanayowasumbua kutoka kwa wataalamu wa magonjwa husika.
Kwa upande wake Frank Karia ambaye ni makazi wa Mwanza alisema alipewa Rufaa kutoka hospitali ya rufaa ya Bugando na kufika JKCI siku ya Jumatatu ambapo kulikuwa na punguzo la bei na kubahatika kufanyiwa vipimo vya ECHO na ECG baada ya kufanyiwa vipimo aligundulika kuziba kwa mishipa miwili inayopeleka damu kwenye moyo.
“Baada ya kukutwa na tatizo ndani ya wiki moja tayari nimeshazibuliwa mshipa mmoja wa damu na hali yangu inaendelea vizuri kama unavyoniona, baada ya wiki mbili nitarudi kliniki . Leo tarehe 29/03/2019nimeruhusiwa kwenda nyumbani, kwa kweli sikutegemea kama ningepata huduma hii kwa kipindi cha wiki moja” alisema Karia.
Alisema huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo ni za kimataifa na kuwaomba waendelee kutoa elimu kwa umma ili wananchi wafahamu zaidi huduma zinazotolewa.