Na: Lilian Lundo
Taasisi isiyo ya Kiserikali inayojihusisha na utafiti wa maadili ya wanafunzi Shule za Msingi na Sekondari hapa nchini, “Maadili Centre” imeshauri Wanafunzi wanaopata mimba kutorudi shuleni badala yake watafutiwe program nyingine za masomo kama vile masomo ya ufundi katika vyuo vya VETA.
Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Florentina Senya ameyasema hayo leo, Jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya maoni mbalimbali yaliyokusanywa na taasisi hiyo kuhusu mtoto akipata mimba, mara anapojifungua aruhusiwe aendelee na masomo au la?
“Msimamo wa Maadili Centre ni kwamba haiwezekani wanafunzi wanaopata mimba wakiwa shuleni kuendelea na masomo,” amesema Senya.
Amesema kuwa, utafiti unaonyesha watoto ambao wamepata ujauzito hawako tayari kurudi katika Shule walizokuwa wakisoma kutokana na kujiona tofauti na wenzao, kutojiamini na kuwa na woga.
Aidha amesema, suluhisho la kuwasaidia watoto hao kuendelea na masomo ni kujiunga na vyuo vya ufundi ambako watapata ujuzi mbalimbali kama vile kushona na kutengeneza bidhaa kama vile sabuni na thamani, utakaowasaidia katika kujikumu na maisha.
Senya ameeleza baadhi ya maoni waliokusanya kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu, wamehoji kuwa Sheria za Shule zote nchini zinaeleza mwanafunzi kufanya mapenzi ni kosa la kufukuzwa Shule, hivyo kuruhusu kurudi shule kwa mwanafunzi aliyepata mtoto ni kutoa ruksa kwa wanafunzi kufanya mapenzi.
Aidha Senya alitolea mfano wa dada anayeitwa Joyce Mbelwa wa Bagamoyo, Pwani ambaye alipata mimba akiwa kidato cha pili, amesema baada ya kujifungua hakuona uhuru wa kuendelea na elimu, kwani alijiona ni mama na alikuwa na majukumu ya kumlea mtoto wake.
Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Rosaline Castillo amesema, kumekuwa na mmomyoko mkubwa wa maadili kwa watoto wengi wa Kitanzania kutokana asilimia kubwa ya wazazi kutelekeza watoto wao katika kutoa malezi ambapo imefikia mahali watoto wanaitwa “watoto wa siku hizi”.
Amesema kuwa Maadili Centre iko katika mpango wa malezi na maadili ambapo inatarajia kuanzisha maadili club katika shule za Msingi na Sekondari nchini ambapo wanafunzi watapatiwa maarifa ya kujitambua, kujikubali, kujitunza, kujiheshimu, kujiamini na kujilinda.