Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wanachuo DUCE Wajitolea Kufundisha Masomo ya Sayansi Sekondari
Aug 11, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_8915" align="aligncenter" width="750"] Mjumbe wa kampeni ya “Tanzania ya Viwanda Inawezekana”, Bw. Ngenda Nkwabi (kulia) akieleza kampeni hiyo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema hii leo jijini Dar es Salaam katikati ni mwanzilishi wa kampeni hiyo Bw. Emijidius Cornel na kushoto ni Mwanafunzi wa Uandishi wa Habari, ambaye yuko kwenye mafunzo kwa vitendo Idara ya Habari (MAELEZO) Neema Mathias. (Picha na Paschal Dotto -MAELEZO)[/caption]

Na: Neema Mathias

Wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Tanzania (DUCE) Wameiunga mkono kauli ya Rais John Pombe Magufuli ya Tanzania ya Viwanda kwa kujitolea kufundisha masomo ya Sayansi kwa baadhi ya shule za Sekondari Wilayani Temeke.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini  Dar es Salaam. , Mwenyekiti wa kampeni ya “Tanzania ya Viwanda Inawezekana”, Emijidius Cornel amesema wanachuo wa DUCE wameamua kutumia muda wao wa ziada kufundisha masomo ya sayansi kwa shule za sekondari.

“Waalimu wa masomo ya sayansi tumeamua kujitolea kufundisha bila malipo masomo hayo katika baadhi ya shule za sekondari ambazo zina upungufu wa waalimu wa sayansi, kwani maendeleo ya viwanda yanahitaji wataalamu,” alisema Cornel.

[caption id="attachment_8916" align="aligncenter" width="750"] Mwanzilishi wa kampeni ya “Tanzania ya Viwanda Inawezekana” Bw. Emijidius Cornel (katikati) toka Chuo cha DUCE akionesha kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) baadhi ya michoro iliyochorwa na wanafunzi wanaowafundisha kwa kujitolea, kulia ni Ngenda Nkwabi mjumbe wa zoezi hilo na kushoto ni Mwanafunzi wa Uandishi wa Habari ,ambaye yuko kwenye mafunzo kwa vitendo Idara ya Habari (MAELEZO) Neema Mathias.[/caption]

Mwenyekiti huyo alisema kuwa, walianza kujitolea rasmi Februari 16, 2017 kwa lengo la kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kuhamasisha wanafunzi kuyapenda na kuyapa kipaumbele masomo ya Sayansi shuleni ili kuongeza ufaulu wa masomo hayo.

Aidha, Cornel alieleza kuwa wameanzisha matamasha kwa shule za sekondari Temeke yatakayo fanyika Oktoba 6 na Novemba 18 mwaka huu, kwa lengo la kuendelea kuwapa moyo wanafunzi kupenda masomo ya Sayansi.

Hata hivyo, Mwenyekiti huyo ameiomba  Serikali na wadau wengine wenye uzalendo na nchi yao kuchangia  na kuunga mkono kampeni hiyo, kwani muda mwingine wanakumbana na changamoto  mbalimbali ikiwemo nauli  za kuwafikia wanafunzi walioko  kwenye shule za mbali na maeneo ya chuo .

“Tunaiomba Serikali pamoja na wadau mbalilmbali watuunge mkono katika suala hili kwani tumeanza kwa moyo mkunjufu na tunaomba tusikwamishwe na mtu yeyote yule, kwa wanotaka kutuunga mkono wanaweza kuwasilisha michango yao kupitia akaunti namba 20701100005 NMB yenye jina la Kibasila Sekondari, tawi la Temeke au kupitia namba 0718883718”, alieleza Cornel.

Pia ameiomba Serikali kutoa hamasa kwa vyuo vingine vya Ualimu nchini kufanya kazi ya kujitolea kufundisha wanafunzi shuleni katika manispaa mbalimbali ili kukabiliana na changamoto ya waalimu wa masomo ya Sayansi kote nchini.

Kwa upande wake, Mjumbe wa kampeni hiyo, Ngenda Nkwabi amewataka vijana kuwa wazalendo na kuacha kutumia muda mwingi kuchati kwenye mitandao ya kijamii na kufanya mambo yasiyo ya msingi, badala yake kutumia muda huo kutoa elimu kwa wanafunzi walioko shuleni katika ngazi za elimu ya sekondari.

Aidha, Nkwabi alisema kuwa anaamini wanafunzi wengi wanapenda masomo ya Sayansi lakini kutokana na kukosekana kwa waalimu wa kutosha katika shule nyingi wanafunzi hao huishia kuona ugumu na kuyachukia masomo hayo, hivyo anaiomba Serikali kuwapa ushirikino katika kampeni hiyo ili kumaliza kabisa tatizo hilo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi