Wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) mkoani Mwanza, wameupongeza Mfuko huo kwa kuwa karibu na Wanachama wake na kuendelea kutoa huduma bora.
Pongezi hizo zimetolewa na Wanachama hao jijini Mwanza Oktoba 5, 2023 wakati wa shamrashamra za wiki ya huduma kwa wateja ambayo inaadhimishwa wiki hii ulimwenguni kote.
Katika kuhakikisha PSSSF inapata mrejesho sahihi kutoka kwa wanachama wake, Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji, Bw. Fotunatus Magambo aliongoza timu ya Maafisa wa PSSSF kuwatembelea wanachama katika ofisi zao na wastaafu katika makazi yao.
Wakiwa katika ofisi za Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Mwanza (MWAUWASA), walikutana na Watumishi watatu ambao wote walisema wanafurahishwa na huduma za PSSSF.
“Kwa kweli mimi wakati nimejifungua sikupata shida kupata fao la uzazi, nililipata kwa wakati, hata hivyo nawashauri wakina Mama wengine kuhakikisha wanawasilisha nyaraka zote muhimu ndani ya miezi mitatu baada ya kujifungua ili waweze kupata fao hilo”, alifafanua Bi. Monika Emmanueli, Mtumishi wa MWAUWASA.
Naye Bi. Vumilia Jonas, Mtumishi MWAUWASA alishauri, “Ni vyema PSSSF iweke mfumo wa kutoa mrejesho wa Wanachama ili waweze kujua nini kinaendelea katika huduma inayofuatiliwa na mwanachama”.
PSSSF ina huduma mbalimbali za kumwezesha mwanachama kufuatilia huduma jambo lolote juu ya uanachama wake, moja ya huduma hiyo ni PSSSF kiganjani ambapo wanachama wanaweza kuhudumiwa kupitia simu janja bila ya kuhitaji kufika kwenye Ofisi za Mfuko.
Pia Bw. Magambo na timu yake walimtembelea Daktari Msataafu wa Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana, Dkt. Gervas Manzi ambaye anaishi Nyamagana jijini Mwanza kwa lengo la kumjua hali na kupata mrejesho wa huduma za PSSSF kwa wastaafu.
“Kwa kweli huduma za Mfuko zipo vizuri, kwa upande wangu nipo vizuri sana na pensheni yangu naipokea kwa wakati, hata hivyo nashauri PSSSF iendelee kutoa elimu kwa wanachama ili waweze kujua haki zao kabla na baada ya kustaafu”, alishauri Dkt. Manzi.
Wiki ya huduma kwa wateja huadhimishwa kila wiki ya kwanza ya Oktoba, lengo lake ni kuzikumbusha taasisi mbalimbali kutoa huduma bora na za wakati kwa wateja wake.