Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wakurugenzi Watakiwa Kusimamia Maadili Katika Sehemu Zao za Kazi
Mar 21, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Eleuteri Mangi-WUSM, Dodoma

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewaagiza Wakuu wa Idara na Vitengo vya Wizara hiyo kusimamia kwa dhati suala la maadili katika sehemu zao za kazi.

Maagizo hayo yametolewa na Waziri Mchengerwa alipokuwa akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo ambacho kinafanyika kwa siku mbili kuanzia Machi 21-22, 2022 Jijini Dodoma.

Waziri Mchengerwa amewahimiza watumishi wa wizara hiyo kutumia muda wao wa kazi kuwahudumia wananchi kwa kujibu hoja za wananchi na kutatua kero zao kwa haraka na ufanisi.

Hatua hiyo itawasaidia watumishi hao kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuongeza bidii kazini, uadilifu, uwajibikaji pamoja na kuzingatia Sheria ambayo ni msingi wa utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe.  Rais Samia Suluhu Hassan.

“Mimi kama Waziri mwenye dhamana ya kusimamia Wizara hii, sitamuonea haya, wala kufumbia macho vitendo vyovyote vinavyoashiria uzembe, ukiukwaji wa haki, upendeleo, rushwa ama ufanyaji kazi kwa mazoea”, amesema Waziri Mchengerwa.

Akinukuu Ripoti ya Tume ya Kero ya Rushwa nchini 1996:168, Waziri Mchengerwa amesisitiza “Tatizo la rushwa miongoni mwa watumishi wa Serikali haliwezi kuondolewa bila kuwa na uongozi imara na usiosimamia utendaji wa kazi ipasavyo, Wasimamizi wa kazi wenye uwezo, uadilifu, wabunifu wenye mienendo na tabia nzuri”.

Katika kudhihirisha umuhimu wa utendaji bora wa kazi kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, Waziri Mchengerwa amemnukuu Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin Mkapa akihutubia Bunge mwaka 1995 aliwahi kusema “Maneno matupu japo yawe matamu kiasi gani hayawezi kumaliza rushwa. Ushirikiano na kila mmoja kutimiza wajibu wake katika vita hivi, ndiyo mwanzo wa mafanikio” 

Awali akitoa mada kwa wajumbe wa Baraza hilo, Bi. Tulia Nsemwa mwakilishi kutoka Ofisi  ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu amewasisitiza wajumbe hao kuwa wanawajibu wa kufanya kazi kwa umoja kama timu hatua itakayosaidia kufikia dira ya Wizara inayolenga kuwa na taifa lenye kuendeleza utambulisho wa taifa kwa kuwawezesha vijana kiuchumi, kukuza utamaduni na michezo kwa umma kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi