Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wakurugenzi Songwe Waipongeza Serikali Maboresho Miundombinu ya Elimu
Jan 30, 2024
Wakurugenzi Songwe Waipongeza Serikali Maboresho Miundombinu ya Elimu
Muonekano wa moja ya shule zinazojengwa na Serikali nchini
Na Jacquiline Mrisho – Maelezo

Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya katika Mkoa wa Songwe wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu msingi na sekondari kwa kuwa imepelekea kuongeza udahili wa wanafunzi, imepunguza mdondoko na imeboresha mahudhurio ya wanafunzi na kupelekea ufaulu kuongezeka.

Pongezi hizo zimetolewa leo mkoani Songwe wakati wa mkutano wa Waandishi wa Habari na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Dkt. Francis Michael pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri ikiwa ni muendelezo wa Programu ya “TumewasikiaTumewafikia” iliyoandaliwa na Idara ya Habari – Maelezo inayotarajiwa kuifikia mikoa yote Tanzania Bara.

Mkurugenzi wa Halmashauri  ya Wilaya ya Ileje, Nuru Kindamba amesema kuwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, halmashauri hiyo imepokea jumla ya shilingi 30,432,407,727 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo katika sekta ya elimu, shule za sekondari za serikali zimeongezeka kutoka shule 19 hadi 22 mwaka 2024 ambapo vimejengwa vyumba vya madarasa 267 kutoka vyumba 205 vilivyokuwepo mwaka 2021. Aidha, idadi ya mabweni imeongezeka kutoka 8 mwaka 2021 hadi 14 mwaka 2024.

“Mwaka 2021 kuna shule zilikuwa na umbali mrefu kwa wanafunzi, kati ya shule za sekondari za serikali 22, shule 3 zimejengwa kwa  dhumuni  la kupunguza umbali kwa wanafunzi kwenda shuleni, kwa upande wa elimu msingi, shule zilikuwa 84 kwa sasa zimefikia 88, mwaka 2021 vyumba vya madarasa vilikuwa 541 na kwa sasa vimeongezeka kufikia 620. Ongezeko la miundombinu hiyo limesaidia kuweka mazingira wezeshi ya kusomea hivyo kuongeza ufaulu”, amesema Mkurugenzi Kindamba.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba, Fabian Said ameeleza kuwa, idadi ya shule za msingi zimengezeka kutoka 75 hadi 95 huku idadi ya madarasa ikiongezeka kutoka 490 hadi 618. Aidha, idadi ya Shule za Sekondari imeongezeka kutoka 11 hadi 16 ambapo madarasa yake yameongezeka kutoka 109 hadi 217.

“Ongezeko la miundombinu ya shule limeboresha ufaulu, limepunguza kero ya umbali wa shule, limeongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga, imepunguza idadi ya wanafunzi wanaoacha shule kwa sababu mbalimbali na limeboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia”, amesema Mkurugenzi Said.

Nae, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Abdallah Nanonde amesema kuwa, halmashauri ilipokea shilingi bilioni 3.28 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya elimu msingi ambapo imefanikiwa kukamilisha jumla ya vyumba vya madarasa 73 ikiwemo 67 vya kawaida na 6 vya elimu ya mfano katika shule za msingi 20.

“Kwa upande wa shule za sekondari, halmashauri ilipokea bilioni 6.75 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo madarasa 246, maabara 26, maktaba 6, majengo ya TEHAMA 6, majengo ya utawala 6 na nyumba za walimu 6.  Kabla ya Serikali ya Awamu ya Sita kuingia madarakani, shule za sekondari zilikuwa 45 na sasa zimefikia 52  huku shule za msingi kufikia 186 kutoka 179”, amesema Mkurugenzi Nanonde.

CPA Cecilia Kavishe, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe amefafanua kuwa kabla ya Serikali ya Awamu ya Sita kuingia madarakani, idadi ya shule za sekondari za serikali zilikuwa 11 na kwa sasa zimepanda hadi 16 hali iliyopelekea kupunguza mdondoko na ufaulu kuongezeka. Madarasa yameongezeka kutoka 131 hadi madarasa 261. Vile vile, idadi ya shule katika elimu msingi imeongezeka kutoka 58 hadi 62 hali iliyopelekea ongezeko la udahili wa wanafunzi kutoka 31,041 hadi 45,326.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Belton Gagiro ameeleza kuwa halmashauri hiyo imejenga jengo la ghorofa lenye jumla ya vyumba vya madarasa 10, ofisi 4 za Walimu na matundu 24 ya vyoo katika shule ya msingi HISOJA, imejenga jengo la ghorofa lenye jumla ya vyumba vya madarasa 10, ofisi 4 za Walimu na matundu 24 ya vyoo, jengo la utawala na nyumba 2 (2/1) katika shule ya msingi Kokoto ambapo majengo hayo yapo katika hatua ya umaliziaji huku vyumba 5 vya madarasa yaliyokamilika tayari yameshawapokea wanafunzi.

Vile vile, ameeleza kuwa zimejengwa shule 2 mpya za msingi katika Mitaa ya Isanzo na Namazanya,  shule mpya ya sekondari Chipaka na shule mpya ya sekondari Dr. Samia S. H ambayo jengo la utawala, nyumba 2 za Walimu, mabweni 2 na jengo la ghorofa lenye jumla ya vyumba 5 vya madarasa, ofisi 2 za Walimu na matundu 24 ya vyoo yamekamilika. Majengo mengine ya jengo la ghorofa lenye vyumba 16 vya madarasa, ofisi 5 za Walimu, matundu 32 ya vyoo, majengo ya maabara 2, mabweni 3 na nyumba 3 za walimu yanaendelea na ujenzi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi