Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wakulima watumia hatimiliki za kimila kukopa benki bilioni 18.9
Jan 28, 2021
Na Msemaji Mkuu

Mmoja wa Wakulima wa mpunga wilayani Mbarali mkoani Mbeya  walionufaika na urasimishaji ardhi Bw. Paulinus Msigwa akionesha   Kamati ya Uongozi ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA) manufaa alliyopata  ikiwemo matrekta aliyonunua baada ya kurasimisha mashamba yake na kupatiwa hatimilki za kimila za kumiliki ardhi. Kamati hiyo imeongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Balozi (Mstaafu) Daniel Ole Njoolay imewatembelea baadhi ya wanufaika wa mpango wilayani humo.

Na Mwandishi Wetu- Mbarali

Taasisi za fedha zikiwemo Benki za CRDB na NMB wilayani Mbarali katika Mkoa wa Mbeya, zimekopesha wananchi shilingi bilioni 18.09 baada ya kurasimisha mashamba yao na kupatiwa hatimilki za kimila za kumiliki ardhi katika msimu wa mwaka 2014/2015 na 2019/2020.

Akizungumza na baadhi ya wanufaika wa urasimishaji ardhi baada ya halamshauri kuwezeshwa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA), Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa MKURABITA, Mhe.Daniel ole Njoolay amesema mafanikio hayo ni ishara kuwa, urasimishaji ardhi uliofanywa baada ya MKURABITA kujenga uwezo umezaa matunda yaliyokusudiwa. 

"Manufaa ya hatimilki za kimila za kumilki ardhi ni makubwa na yameleta tija hivyo niwasihi wananchi wote kutumia fursa hii kujikwamua kiuchumi na pia, taasisi nyingi zaidi za fedha zije katika maeneo haya na kuwawezesha wananchi kwa kutumia hati zao," alisisitiza Mhe. Njoolay.

Mweyekiti wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA  Mhe. Balozi (Mstaafu) Daniel Ole Njoolay (Wakwanza kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati hiyo na wanufaika wa mpango huo kabla ya kuanza ziara yakutembelea maeneo yao kujionea jinsi urasimishaji ulivyoleta tija katika uzalishaji kupitia sekta ya kilimo Wilayani Mbarali.Wa pili kutoka kushoto  ni Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Gabriel   Mfune.

Amesema urasimishaji ardhi katika maeneo ya wakulima na wafugaji umekuwa mkombozi wa kiuchumi uliowawezesha wengi kusomesha watoto, kuongeza tija kwenye katika shughuli zao, kuondoa migogoro ya ardhi na kukua kiuchumi.

Kwa upande wake, Mratibu wa MKURABITA Dkt. Seraphia Mgembe, amesema Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali imeonesha mfano bora katika kuendeza dhana ya urasimishija ardhi baada ya kujengewa uwezo na MKURABITA. 

Aidha, Dkt. Mgembe ametoa mwito kwa taasisi za fedha kuunga mkono juhudi za serikali kuboresha huduma za jamii na kuchochea maendeleo kwa kurejesha kwa jamii sehemu ya faida ziipatayo kwa kuchangia na kusaidia mambo mbalimbali.

Alisema hatua hiyo itachochea maendeleo ya jamii katika sekta ya ardhi hasa urasimishaji ardhi na ujenzi wa miundombinu zikiwamo masjala za vijiji kwa ajili ya kutunzia hatimiki za kimila za kumiliki ardhi kwani hali hiyo pia itawafanya wananchi kuziona taasisi hizo kuwa ni zao na kuzitumia zaidi kwa akiba na mikopo. 

Moja ya matrekta yanayomikiwa na  Bw. Paulinus Msigwa ambaye ni mmoja wa wanufaika wa urasimishaji ardhi uliofanywa baada ya MKURABITA kujenga uwezo kwa Halmashauri ya Wilaya  ya Mbarali Mkoani Mbeya ili kuwezesha wananchi kunufaika na urasimishaji ardhi na kupatiwa hatimilki za kimila.

Naye Ofisa Ardhi na Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Bw. Geofrey Mwaijombe, alisema halmashauri hiyo imekuwa ikiendelea urasimishaji arhi na kufanikiwa kupima mashamba 2,953 sambamba na kutoa hatimilki za kimila 2,720 katika vijiji yake mbalimbali.

"Tunashirikisha wadau katika urasimishaji baada ya MKURABITA kujenga uwezo kwa halmashauri na mwezi Februari 2021, tunatarajia kuanza urasimishaji katika Vijiji vingine 10 lengo likiwa kupima kila kipande cha ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali. 

Mwaijombe alisema Vijiji vyenye mpango wa matumizi bora ya ardhi vimeongezeka kutoka 16 mwaka 2009/2010 hadi kufikia 36 mwaka 2020/2021.

Akieleza mafanikio yatokanayo na urasimishaji, Mwaijombe amesema ni pamoja na wananchi kuanzishwa kwa viwanda vya kuongeza thamani mazao, ujenzi wa makazi bora na  kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao. 

MKURABITA imejenga uwezo kwa halmashauri mbalimbali nchini ili kutekeleza kwa vitendo, dhana ya urasimishaji ardhi na biashara kwa wananchi ili wajikwamue kiuchumi.

Mratibu wa MKURABITA Dkt. Seraphia Mgembe akieleza faida wanazopata wananchi waliorasimisha mashamba yao na kupatiwa hatimilki za kimila za kumiliki ardhi Wilayani Mbarali mkoani Mbeya wakati wa ziara ya Kamati ya Uongozi ya MKURABITA inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Balozi (Mstaafu) Daniel ole Njoolay.

Mmoja wa Wakulima wa mpunga wilayani Mbarali mkoani Mbeya  walionufaika na urasimishaji ardhi Bw. Paulinus Msigwa (Wa kwanza kulia) akisisitiza jambo kwa  Kamati ya Uongozi ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA) ikiwemo matrekta aliyonunua baada ya kurasimisha mashamba yake na kupatiwa hatimilki za kimila za kumiliki ardhi. Kamati hiyo imeongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Balozi (Mstaafu) Daniel Ole Njoolay kuwatembelea baadhi ya wanufaika wa mpango huo wilayani humo.

(Picha na MAELEZO)

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi