Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wakulima Wapewa Siku Sita Kukamilisha Mifereji ya Maji Mashambani Mwao
Nov 13, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Tiganya Vincent, RS –Tabora

Wakulima wa Mpunga katika Mradi wa Umwagiliaji wa Ussoke Mlimani na Yelayela ambao hadi hivi sasa hawajakamilisha uchimbaji wa mifereji ya kusambaza maji kutoka mfereji mkuu kwenda kwenye mashamba yao wametakiwa kuhakikisha wamekamilisha zoezi ndani ya wiki hii.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni katika eneo la mradi la Ussoke Mlimani na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Margaret Nakainga wakati wa kikao kati ya Uongozi wake na Wakulima wanachama mradi huo wa umwagiliaji.

Alisema kuwa baada ya muda waliokubaliana katika kikao hicho kumalizika, watakaokuwa wameshindwa watachukuluiwa hatua na viongozi wao kulingana na maamuzi waliyokubaliana ili wasiendelee kuwa kikwazo cha kutaka kurudisha nyuma ufanisi wa mradi huo uliotumia fedha nyingi.

Nakainga alisisitiza kuwa ucheleweshaji wowote unaweza kusababisha baadhi ya wakulima washindwe kulima kwa sababu ya mkulima aliyemtangulia hajachimba mfereji ambao utaruhusu maji yapite kwake kisha yaende kwa jirani yake.

“Natarajia kuja kukagua siku ya Ijumaa kama mtakuwa mmekamilisha kuchimba mifereji kama tulivyokubaliana katika kikao hiki atakayekuwa hajakamilisha tutaona ni hatua gani tuchukue ili asije akawa kikwazo kwa wanamradi wengine” alisisitiza Mkurugenzi huyo.

Naye Mwenyekiti wa Mradi huo Bryson Kazala aliwataka wakulima ambao hawajakamilisha maandalizi ya mashamba yao kufanya hivyo mapema la sivyo watalazimika kuwanyang’anya na kuwagaiwa waliotayari kuyaendeleza.

Alisema kuwa lengo la mradi huo ni kutaka kila eneo lililopimwa lifanyekazi ya uzalishaji ili hatimaye waweze kuishawishi Serikali ipanue eneo la mradi kwa ajili ya kuingiza wanachama wengi zaidi.

Kazala alisema kuwa ni vyema kila mkulima aliyeomba shamba na kupatiwa akahakikisha ndani ya muda waliojipangia anaweka eneo lake vizuri tayari kwa ajili ya kilimo.

Kwa upande wa Katibu wa Mradi huo Rajab Karunguyeye alisema kuwa ikiwa wanachama waliojiandikisha katika mradi huo watawajibika ipasavyo wataondoa suala la kuagiza mchele kutoka nje ya kijiji na kuwa na ziada ya kuwauzia watu wengine.

Mradi huo ambao umegharimu zaidi ya shilingi milioni 800 una mashamba ambayo yana ukubwa wa hekta 211 ambayo ni kwa ajili ya kilimo cha kisasa cha umwagiliaji mpunga.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo alitoa wito kwa Wakulima wote wilayani humo kutumia mvua zilizoanza kunyesha kulima mazao mazao mchanganyiko kwa ajili ya chakula na biashara.

Alitaja baadhi ya mazao hayo kuwa ni mihogo, viazi vitamu, mahindi , alizeti , pamba, karanga na tumbaku kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wanakuwa na mazao ya aina mbalimbali ambayo yatakuwa chanzo cha chakula na wanaweza kuyauza kwa ajili ya uboreshaji wa maisha, pia aliwataka wanapolima wazingatie ushauri wa wataalam ili waweze kupata mazao bora.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi