Wakulima wanaonufaika na Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na kuongeza usalama wa chakula katika maeneo kame Tanzania (LDSF) wamepatiwa mafunzo kuhusu teknolojia za kilimo hifadhi na kinachohimili mabadiliko ya tabianchi.
Mafunzo hayo yamefanyika katika Halmashauri ya Kondoa mkoani Dodoma kupitia mradi huo unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais yametolewa kwa wakulima kutoka vijiji vya Halmashauri za Wilaya za Mkalama (Singida), Magu (Mwanza), Nzega (Tabora) na Micheweni (Unguja).
Mratibu wa Mradi wa LDSF kutoka ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Joseph Kihaule alisema wakulima wamejifunza teknolojia za kilimo hifadhi cha Mbegu Tisa na Jembe la Mzambia ambayo imeonesha matokeo mazuri kwa mashamba darasa ya vijiji vya Haubi na Mafai katika Halmashauri ya Kondoa.
Bw. Kihaule alifafanua kuwa teknolojia za kilimo cha Mbegu Tisa na Jembe la Mzambia zinasaidia kurutubisha ardhi na kutunza unyeunvevu kwa muda mrefu na kwa mvua chache.
Alisema kuwa katika uzalishaji na kurejesha ardhi unafanyika kibaiolojia kwa kutumia samadi pamoja na kuendeleza mifumo ikolojia ili kupata mvua na kurutubisha ardhi kwa njia ya kuchimba mabwawa, malambo na visima virefu kwa ajili ya umwagiliaji.
Aidha, mratibu huyo alibainisha kuwa tayari hati miliki za kimila 1,700 kati ya 2,100 ya walengwa hatua ambayo ni chachu kwa halmashauri ili ziendele kutoa hati miliki za kimila hivyo kutunza mazingira badala ya kilimo cha kuhama.
Wakizungumza mara baada ya mafunzo hayo, baadhi ya wakulima akiwemo Zakaria Pamba kutoka Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, alisema wamejifunza mbinu mbalimbali za kilimo.
Pia wakulima Restuta Deogratius na Julius Mponeja wa Wilaya ya Nzega mkoani Tabora mafunzo hayo yamesaidia kupata elimu ya kilimo bora ambayo itasaidia katika kuwapatia mazao ya kutosha.
Bi. Theresia Emanuel, mkulima wa Kijiji cha Haubi Maziwani wilayani Kondoa alisema kabla ya kuletewa teknolojia hiyo walipokuwa wanalima walipata mavuno kidogo lakini hivi sasa kiwango cha mazao kimeongezeka.