Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mil. 16.5 Kukamilisha Ujenzi Kituo cha Polisi Bonde la Ziwa Rukwa
Apr 09, 2018
Na Msemaji Mkuu

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joachim Wangabo amekabidhi shilingi milioni 5 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa alipotembelea ujenzi wa kituo hicho cha polisi tarehe 13.11.2017 na wananchi kumuomba kuchangia ambapo ukamilifu wa kituo hicho utasaidia kuhudumia kata 13 zilizopo katika bonde la ziwa Rukwa.

Sambamba na hilo Mhe. Wangabo pia aliwasilisha ahadi ya Milioni 10 aliyoitoa Mkuu wa jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro alipotembelea Mkoa wa Rukwa na kuongeza kuwa kuna shilingi milioni 1.5 ambayo pia ni ahadi ya mkazi wa bonde la ziwa Rukwa anayeishi nje ya Mkoa ambaye hakuhitaji kutajwa jina lake.

“Nimekuja kutekeleza ahadi yangu ambayo inaendana na mlichonisomea, mlisema ili kituo cha polisi kikamilike mlihitaji shilingi milioni 4, mkaniomba niwatafutie, mimi nimekuja na shilingi milioni 5, ila nilituma timu yangu ili kuangalia ile gharama kama ilikuwa sahihi, nikaambiwa na hiyo timu kuwa inahitajika shilingi Milioni 22, alipokuja Kamanda IGP niliteta nae na alipoona umuhimu wa kituo hiki aliahidi shilingi Milioni 10,” Mhe. Wangabo alisema.

Wakati akikabidhi fedha hizo kwenye mkutano na wananchi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Albinus Mgonya alimtaka Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Hamis Mongela kukiri kupokea fedha hizo huku ahadi nyingine zikiendelea kufuatiliwa ili ujenzi wa kituo hicho ukamilike kwa wakati.

Diwani wa kata ya Mtowisa Mhe. Edgar Malinyi alisema kuwa ujenzi wa kituo hicho ni juhudi za wananchi wanaotaka usalama wa vitu na mali zao wakishirikiana na polisi huku mtendaji wa Kata ya Mtowisa,Paulo Katepa akisema kuwa wananchi hawatakata tamaa hadi kituo hicho kikamilike kwani ujenzi wake ulioanza tangu mwaka 2002.

IMETOLEWA NA

OFISI YA MKUU WA MKOA WA RUKWA

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi