Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mheshimiwa Moses Kahegele amewataka wakandarasi wazawa kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi ili kuweza kulisaidia Taifa na kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere.
Ameyasema hayo leo tarehe 19/01/2024 wakati alipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi unaondelea katika Kampasi Kuu ya Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia.
“Nitoe rai kwa wakandarasi wazawa wanaopata kazi katika Wilaya ya Butiama, wafanye kazi kwa wakati na ubora ili Serikali iweze kuwapa miradi mingi na mikubwa”, ameshauri Mheshimiwa Kahegele.
Mheshimiwa Kahegele ameonyesha kusikitishwa na hali ya kuchelewa kwa shughuli za ujenzi kwa wakandarasi wawili kati ya watatu wanaotekeleza ujenzi huo.
“Huu ni mradi mkubwa sana lakini kwa wakandarasi wawili ambao wamechelewa kwa wiki tatu imenisikitisha sana. Nimewaagiza wafanye kazi usiku na mchana ili kufidia muda uliopotea,” amesisitiza Mheshimiwa Kahegele.
Mheshimiwa Kahegele amempongeza mkandarasi mmoja ambaye amefanikiwa kutekeleza shughuli za ujenzi ndani ya muda uliopangwa.
Aidha, Mheshimiwa Kahegele amemtaka mshauri mwelekezi kuwepo katika eneo la ujenzi muda wote ili kuhakikisha ujenzi unafanywa kwa viwango stahiki na kuepusha ujenzi wa majengo ulio chini ya kiwango.
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Fedha, Mipango, na Utawala, Prof. Msafiri Jackson amemuhakikishia Mkuu wa Wilaya ya Butiama kuwa chuo kwa kushirikiana na mshauri mwelekezi kitahakikisha maelekezo yaliyotolewa yanafanyiwa kazi.
“Tutahakikisha wakandarasi wanafanya kazi vizuri na kwa ubora na kuhakikisha muda uliopotea unafidiwa kwa kuweka mikakati sahihi wakati huo huo wakiendelea na kazi zilizokuwa zimepangwa kwa wakati huu” amesema Prof. Jackson.
Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia kinatekeleza ujenzi wa majengo 16 katika Kampasi Kuu Butiama, ujenzi unaogharamiwa na Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ambao unatarajiwa kukamilika Mei 30, 2025.