Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wakandarasi Umeme wa Makambako-Songea watakiwa kukamilisha kazi
Aug 16, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Teresia Mhagama, Njombe

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani amewataka wakandarasi waliopewa kazi ya kujenga vituo vya kupoza Umeme na kazi ya kusambaza Umeme katika Mradi mkubwa wa usafirishaji Umeme wa Makambako - Songea kukamilisha kazi hizo ifikapo septemba mwaka huu.

Dkt. Kalemani aliyasema hayo leo katika Mji wa Makambako mkoani Njombe wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo ambao unahusisha ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji Umeme wa msongo wa kV 220, Vituo vipya vya kupoza umeme, upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Makambako na  Usambazaji umeme.

Akizungumza kuhusu Mkandarasi, kampuni ya JV Shandong Taikai Power,  Dkt Kalemani alisema kuwa, kampuni hiyo ilipewa kazi kujenga vituo viwili vipya vya kupozea umeme vya kV 220/33 katika mji wa Madaba na Songea na upanuzi wa kituo cha kupozea umeme cha Makambako cha kV 220/132/33.

"Kampuni hii ilianza shughuli zake miaka mitatu  iliyopita na  ilitakiwa kukamilisha kazi  Machi 2018 lakini mpaka sasa bado hakuna maendeleo yoyote, hivyo naagiza msitoke katika eneo la kazi mpaka kutakapokuwa na hatua za kuridhisha za ujenzi ," alisema Dkt Kalemani.

Aidha, Dkt. Kalemani alimwagiza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO kuhakikisha kuwa kampuni hiyo haipati malipo yoyote mpaka itakapoanza kufanya kazi husika na tathmini kufanyika.

Kuhusu kazi ya usambazaji umeme katika vijiji 120 vya mkoa wa Njombe na Ruvuma kupitia mradi huo, Dkt Kalemani alimtaka Mkandarasi ambaye ni kampuni ya Isolux Ingenieria kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo ifikapo Septemba, 2017 kwani alitakiwa kukamilisha kazi husika mwezi Desemba 2016.

Alisema kuwa, Mkandarasi huyo atasambaza umeme katika eneo lenye urefu wa kilometa 900 na kuunganisha wateja 22,700 katika mikoa ya Njombe na Iringa na kumwagiza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO kuteua Msimamizi mpya kutoka Shirika hilo atakayesimamia mradi huo ipasavyo.

Kuhusu kazi ya ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji umeme wa msongo wa KV 220 kutoka Makambako hadi Songea wenye urefu wa kilometa 250, Naibu Waziri alisema kuwa kazi hiyo inaendelea vizuri.

"Kampuni ya Kalpataru inayojenga miundombinu hii kwa sasa wanafanya vizuri lakini bado tunawasisitiza kukamilisha kazi hii mwezi Machi, 2017," alisema Dkt. Kalemani.

Kuhusu gharama za mradi, alisema kuwa Serikali ya Sweden ilitoa jumla ya Krona milioni 620 na Serikali ya Tanzania imechangia jumla ya Dola za Marekani milioni 20 na kutoa jumla ya Shilingi Bilioni Saba kwa ajili ya ulipaji fidia kwa watu waliopisha ujenzi wa Miundombinu hiyo ya umeme ya KV220.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kalemani alikutana na Mkuu wa mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka na kuzungumza naye kuhusu miradi mbalimbali ya umeme ikiwemo mradi huo wa Makambako- Songea ambapo alimuomba Mkuu wa Mkoa huyo kuwasimamia kwa karibu wakandarasi hao hasa suala la kuhakikisha kuwa wanakuwepo eneo la kazi.

Aidha, Mkuu wa mkoa wa Njombe alimpongeza Dkt. Kalemani kwa juhudi mbalimbali anazofanya ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma ya Umeme ya uhakika na kuahidi kushirikiana na watalaam mbalimbali wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani humo ili kuhakikisha kuwa wakandarasi wa Umeme wanatekeleza majukumu yao kama ambavyo mikataba inaelekeza.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi