Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wajane Wasikate Tamaa Wanapoondokewa na Wenza Wao – Mama Tunu Pinda
Dec 28, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu, Mama Tunu Pinda amewataka wajane wasikate tamaa ya maisha au kujiona wanyonge pale wanapoondokewa na wenza wao.

Ametoa wito huo mwishoni kwa wiki wakati akizungumza na waumini na watu mbalimbali walioshiriki hafla ya chakula cha mchana cha Krismasi iliyofanyika kwenye Kanisa la Upendo Revival Christian Center (TAG) jijini Dodoma.

"Leo nimejifunza jambo kubwa sana hapa kanisani, kanisa limeonesha upendo wa hali ya juu sana kwa kuweza kukusanya idadi ya watu 500 na kula nao chakula,” alisema kabla ya kutoa zawadi kwa wahitaji waliojumuisha wajane, watoto yatima na watoto wa mitaani.

"Natamani hata mimi kufanya jambo kama hili kwani ni upendo wa aina yake, napenda kusema hili ni tukio kubwa na la kuigwa na watu wote," alisema.

Mama Pinda ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo alisema: "Pamoja na kanisa kuhubiri neno la Mungu, pia limeweza kuwajali watu kimwili kwa kushiriki nao chakula pamoja na mahitaji mbalimbali na kuwafanya wafarijike badala ya kujiona wanyonge kwenye sikukuu hii muhimu."

Kanisa hilo lina utaratibu wa kila mwaka kushiriki chakula na watu wenye uhitaji na mwaka huu Kamati ya Dorcas ya Kanisa hilo iliwakusanya wajane 150 kutoka Veyula, watoto yatima 250 kutoka vituo vya Safina (eneo la Ntyuka) na Shukrani (eneo la Kigwe) na watoto waishio katika mazingira magumu wapatao 100 kutoka maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Dorcas iliyopo katika kanisa hilo, Bi. Annie Maugo, alisema matatizo makubwa ya kuwepo kwa watoto wa mitaani yanasababishwa na vurugu na migogoro ya kifamilia.

Bi. Maugo alisema kanisa hilo limekuwa na utaratibu kula chakula na kutoa zawadi mbalimbali kwa watoto waliopo mashuleni na kutoa misaada mbalimbali kwa makundi hayo zenye thamani ya sh. milioni 25.

"Tumetoa vifaa mbalimbali vya masomo kwa wanafunzi wanaoingia shuleni Januari mwakani na pia tumetoa chakula, sukari, sabuni, mafuta ya kula, miswaki, dawa za meno, vitenge pamoja na mafuta ya kujipaka," alisema na kuongeza kuwa: “Zawadi nyingine ni mabegi ya shule, madaftari, ream za karatasi, rula, penseli na kalamu za wino.”

Amesema lengo kubwa ni kuyafanya makundi hayo yajisikie kuwa ni sehemu ya jamii kwa kujumuika na wenzao ili nao wawe na furaha kama zilivyo familia nyingine.

Naye, Mdala Yulia ambaye ni miongoni mwa wajane walioshiriki chakula cha pamoja kanisani hapo amelishukuru kanisa kwa upendo ambao wameuonesha. "Napenda kulishukuru kanisa kwa kuwa na maono ya kutujali sisi wajane na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na zaidi ni pale ambapo wanatuwezesha kupata mahitaji.

"Pamoja na hayo, wamekuwa wakiwasaidia watoto wetu katika kuwawezesha vifaa vya shule jambo ambalo linatutia moyo kwani tunajengwa kiroho, kimwili na kiakili," alisema.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi