Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Little Hearts ambao wanafadhiliwa na Taasisi ya Al- Murtada ya nchini Saudi Arabia wanatarajia kufanya matibabu ya moyo kwa wagonjwa 80 katika kambi maalum inayotarajia kuanza tarehe 10 – 14/12/2017.
Matibabu yatakayofanyika katika kambi hiyo ni ya upasuaji wa kufungua kifua na upasuaji wa bila kufungua kifua (Catheterization) kwa kutumia mtambo wa Cathlab kwa watoto na watu wazima.
Leo tarehe 08/12/2017 madaktari bingwa wa Moyo wameanza kufanya uchunguzi kwa wagonjwa wote watakaofanyiwa upasuaji. Katika kambi hii ya siku tano tumepanga kufanya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa 30 na upasuaji wa bila kufungua kifua kwa wagonjwa 50. Upasuaji wa kufungua kifua utafanyika zaidi kwa watoto na watu wazima watafanyiwa zaidi upasuaji wa bila kufungua kifua.
Kwa nama ya kipekee tunaishukuru sana Serikali kupitia Balozi wetu wa nchini Saudi Arabia Mhe. Hemedi Mgaza kwa kutoa kibali cha kuingia nchini (Visa) bila malipo kwa wataalamu wetu hawa ambao wamekuja nchini kutoa matibabu ya moyo bure kwa wagonjwa wetu.
Kama mnavyofahamu matibabu ya moyo ni ya gharama hivyo basi tunaendelea kuwahimiza wananchi kujiunga na mfuko wa taifa wa bima ya afya ambao utawasaidia kulipa gharama za matibabu pindi watakapougua na kuhitaji kupata matibabu.
Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano na Masoko
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
08/12/2017