[caption id="attachment_40071" align="aligncenter" width="900"] Muonekano wa kengo jipya la mama na mtoto katika Kituo cha Afya Mkoani, kilichopo katika Halmashauri ya mji wa Kibaha mkoani Pwani [/caption]
Na: Lilian Lundo, MAELEZO, Pwani.
Waganga, Wakunga na Wananchi wa Mkoa wa Pwani wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa hatua inazozichukua kuboresha huduma za Afya kwa kutoa fedha kwa ajili ya upanuzi wa vituo vya afya na ujenzi wa hospitali za Wilaya mkoani humo.
Pongezi hizo zimetolewa na wadau hao wa afya mapema wiki hii, huku wakimpongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa anazozifanya.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Lugoba, Halmashauri ya Chalinze, Dkt. Maganga Kazuri amesema wamepokea shilingi mil. 400 kutoka Serikali kuu ambapo fedha hizo zimetumika kujenga majengo matano mapya kituoni hapo ambayo ni jengo la maabara, upasuaji, mama na mtoto, kuhifadhi maiti na nyumba ya mganga mfawidhi wa kituo hicho.
Amesema maboresho hayo yanawagusa moja kwa moja wao kama watoa huduma pamoja na wananchi ambao kwa sasa wanapata huduma nzuri na za kisasa.
"Tulikuwa tunalazimika kuwapa rufaa wagonjwa kwenda hospitali ya Tumbi au Bagamoyo kutokana na kituo kutokuwa na huduma ya upasuaji lakini kutokana na maboresho haya huduma hiyo inatolewa hapa hapa kituoni," amesema Dkt. Maganga.
Kwa upande wake, Mganga wa Kituo cha Afya Kerege, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Dkt. Nyangasi Gideon amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi anazozifanya katika kuboresha huduma za Afya ambayo imewapa morali wa kufanya kazi na kutoa huduma bora kwa Wananchi.
"Tulianza rasmi ujenzi wa kituo cha Kerege Octoba, 2017 ambapo kilikamilika Machi, 2018 na kuanza rasmi kutoa huduma kwa wananchi wa kata ya Mapinga, Kerege na Kiromo, ambapo baada ya maboresho wakina mama 360 wamejifungua," amesema Dkt. Nyangasi.
Amesema, kabla ya kituo hicho hakijafanyiwa maboresho kilikuwa kikipokea akinamama wawili hadi kumi kila siku.
Aidha amesema, mil. 500 zilizotolewa na Serikali zimejenga maabara, jengo la mama na mtoto, jengo la upasuaji na nyumba ya mganga. Fedha hizo zilibaki na kujenga nyumba ya kuhifadhi maiti na jengo la kufulia.
Nae, Muuguzi Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mkoani, Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Immaculate Sangu amesema maboresho yaliyofanyika kituoni hapo yataondoa msongamano wa wagonjwa ambapo hupokea wagonjwa 350 hadi 400 kwa mwezi.
"Furaha yangu ni kuona kwamba hata wagonjwa tuliokuwa tunawapa rufaa kwenda Tumbi sasa tutawahudumia hapa hapa kutokana na uwepo wa chumba cha kisasa cha upasuaji na chumba cha mionzi". alisema Immaculate.
Vile vile mkazi wa Maneromango, Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Omary Rajab amempongeza Rais Magufuli kwa kukiwezesha Kituo cha Afya cha Maneromango kufanya maboresho makubwa ya kujenga majengo matano kwa ajili ya maabara, upasuaji, kuhifadhi maiti, wodi ya wazazi na nyumba ya mganga.
" Kabla ya maboresho haya yaliyofanyika huduma zilikuwa duni. Lakini kwa sasa vifaa vipo na waganga pia wapo, kwa hiyo hata watu wenye matatizo ya mabusha wanafanyiwa upasuaji hapa hapa," alisema Omary.
Pia, mwanafunzi wa Chuo cha Afya Kibaha, anayefanya mafunzo kwa vitendo Kituo cha Afya Maneromango, Anety Mwandiga amesema uwepo wa vifaa vya kisasa katika vituo vya Afya umemuongezea ujuzi wa namna ya kutumia vifaa hivyo.
"Namshukuru Mhe.Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa maboresho haya ya vituo vya afya inawasaidia madaktari na wakunga kupenda kazi zao na kufanya kazi zao vizuri, pia kuwahudumia vizuri Wananchi," amesema Anety.
Serikali ya Awamu ya Tano chini Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli katika kutimiza ahadi yake ya kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini. Ilipoingia madarakani ilianza uboreshaji huo kwa kuanza na ujenzi wa vituo 44 vya afya na kufuatiwa na vituo 74 na sasa vituo takribani 120 vinaendelea kujengwa maeneo mbalimbali ili kutimiza lengo la kuwa na kituo cha afya kwa kila Kata.
[caption id="attachment_40073" align="aligncenter" width="889"] Jengo la zamani la Kituo cha Afya mkoani kilichopo katika Halmashauri ya mji wa Kibaha mkoani Pwani kama inavyoonekana kabla ya ujenzi wa majengo mapya ya wodi ya mama na mtoto, chumba cha upasuaji, maabara na eneo la kufulia.[/caption] [caption id="attachment_40074" align="aligncenter" width="900"] Jengo la Wazazi (mama na mtoto) katika Kituo cha Afya Kerege Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani kama inavyoonekana katika picha ikiwa ni sehemu ya maboresho katika sekta ya Afya yanayowezesha huduma za upasuaji na maabara kutolewa katika Kituo hicho ambapo upanuzi huo umegharimu shilingi milioni 500 zilizotolewa na Serikali[/caption] [caption id="attachment_40075" align="aligncenter" width="900"] Muonekano wa Kituo cha Afya Kerege Wilayani Bagamoyo mkoani Pwani baada ya ujenzi wa majengo mapya kukamilika na kuboreshwa kwa huduma katika kituo hicho chenye uwezo wa kutoa huduma za mama na mtoto, upasuaji, maabara, kituo hicho kimeanza kutoa huduma machi 2018 na kimeshahudumia kinamama zaidi ya 360. Awali kinamama walikuwa wakipata huduma ya upasuaji Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo. Kituo hicho kitahudumia wananchi zaidi ya 7114[/caption] [caption id="attachment_40076" align="aligncenter" width="900"] Muonekano wa Kituo cha Afya Matimbwa Kata ya Yombo Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani kimeigharimu Serikali Shilingi milioni 400. Kituo hicho kitatoa huduma za upasuaji, maabara, mama, mtoto na kuhudumia zaidi wananchi ya 8783.