Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wafanyakazi 250 wa Halmashauri Wapatiwa Mafunzo ya PlanRep Morogoro.
Aug 16, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Jacquiline Mrisho – Morogoro.

Jumla ya wafanyakazi 252 wa Halmashauri mbalimbali kutoka Mikoa ya Pwani, Morogoro, Kilimanjaro na Arusha wamepata mafunzo ya Mfumo ulioboreshwa wa kuandaa Mpango wa Bajeti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa ujulikanao kama PlanRep yanaoendelea mkoani Morogoro.

Takwimu hizo zimetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Msaidizi wa Miundombinu ya TEHAMA – TAMISEMI, Baltazar Kibola wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii kuhusu mafunzo hayo.

Kibola amesema kuwa mfumo huo sio mpya ila umeboreshwa kwa kuongezewa vitu vya muhimu vitakavyomaliza mapungufu yaliyokuwa yakitokea katika mfumo wa zamani hali iliyosababisha kudhoofika kwa utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Mfumo huu ulikuwa ni mfumo unaojitegemea haukuweza kusambaza taarifa katika ngazi mbali mbali za Serikali wala kushirikisha watoa huduma kutoa mapendekezo yao yatakayoongeza uboreshaji wa mipango na Bajeti za Serikali hivyo kwa kuwa tumeuboresha ni wazi kuwa watumiaji wa mfumo huu wanatakiwa kupewa mafunzo,” alisema Kibola.

Kibola ameongeza kuwa katika mradi huo Ofisi ya Rais, TAMISEMI imejikita katika kuratibu utengenezaji wa mfumo huo, kuandaa mafunzo katika mikoa mbalimbali ambayo imepangwa kwa ajili ya kufanyia mafunzo na kutafuta wataalam wa TEHAMA pamoja na wawezeshaji pia kuhakikisha vifaa vya TEHAMA vinakuwepo.

Nae mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo, Christopher Masaaka amesema kuwa asilimia kubwa ya watumiaji wa mfumo wameyapokea vizuri mafunzo hayo kwani mfumo huo unakwenda kurahisisha uandaaji wa mipango na bajeti zinazoandaliwa kila mwaka ambazo zilikuwa zikitumia muda mwingi na gharama kubwa katika maandalizi yake.

“Washiriki wamefanya vizuri katika mafunzo, wameweza kupanga mipango kutoka ngazi ya Vituo, Idara, Halmashauri, Mikoa hadi Wizara kama majaribio pia wameweza kuandaa na kufanya uchambuzi wa mipango na bajeti kupitia mfumo huo,” alisema Masaaka.

Aidha, Masaaka ametoa rai kwa Serikali kuongeza nguvu na jitihada zaidi kwa kuweka miundo mbinu ya TEHAMA na kutoa mafunzo kwa ajili ya kuwajengea uwezo watumiaji katika ngazi zote ili matumizi ya mfumo huo yakaweze kuleta matunda mazuri.

Mafunzo hayo yameandaliwa kwa ufadhili wa Serikali ya Tanzania na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) chini ya Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3).

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi