Na Jacquiline Mrisho.
Serikali imewataka wadau mbalimbali kushiriki katika juhudi za kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza kwani yameendelea kuwa changamoto kubwa nchini.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha kampeni ya kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza pamoja na maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika katika viwanja vya Shule ya msingi Kinyerezi vilivyopo jijini humo.
Makamu wa Rais amesema magonjwa yasiyoambukiza yameendelea kuua watu kwa kasi katika nchi zinazoendelea Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania hivyo ipo haja ya kuimarisha juhudi za kukabiliana na tatizo hilo kwa kushirikiana na wadau wote nchini.
“Magonjwa yasiyoambukiza yasipodhibitiwa yatapunguza uzalishaji mali,ufanisi mahali pa kazi na hata shughuli za ulinzi na usalama nchini mwetu na hivyo kusababisha kupungua kwa pato la Taifa kwani janga hilo linagharimu Taifa na wananchi wake wakiwemo watu wazima, watoto na vijana”, alisema Mhe.Samia.
Aidha, katika kukabiliana na magonjwa hayo, Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali imeweza kupanua maeneo ya kutolea huduma kwa wagonjwa wa saratani nchini kwa kujenga jengo jipya katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na kuongeza majengo mapya ya huduma za saratani kwenye Hospitali za Rufaa ya kanda ya Bugando mkoani Mwanza.
Ameongeza kuwa, Serikali imejenga Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambayo ni taasisi ya kutibu maradhi ya moyo ambapo kutokana na kujengwa kwa taasisi hiyo Serikali imefanikiwa kuokoa fedha nyingi ambazo zingetumika kuwagharamia wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Kigwangalla amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa Wizara hiyo itaendelea kuweka mipango na mikakati imara ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza nchini.
Dkt. Kigwangalla ameomba wadau mbalimbali wakiwemo wa taasisi za kidini na wadau wengine kushirikiana na Wizara hiyo katika kuongeza kasi ya kukabiliana na magonjwa hayo ili yasiendelee kuteketeza maisha ya watanzania.
Kampeni ya kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza imetoa huduma bure za vipimo na matibabu kwa watoto na vijana zaidi ya 1500 na imehitimishwa leo wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika.