Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu Kutembea kwa Miguu Kumuunga Mkono Magufuli
Jul 26, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_7504" align="aligncenter" width="677"] Mwenyekiti wa Shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Young Human Rights Advocates (TYHRA) Samwel Shami akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari kuhusu wachimbaji wadogo wa dhahabu kumpongeza Rais Magufuli leo Jijini Dar es Salaam.[/caption]

Na. Neema Mathias

Wachimbaji wadogo wa dhahabu kutoka wilaya ya Kahama wanatarajia kutembea kwa miguu kutoka Kahama mpaka Dar es salaam kwa ajili ya kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa juhudi zake za  kuijenga Tanzania mpya.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Young Human Rights Advocates (TYHRA) Samwel Shami kwa niaba ya wachimbaji hao, alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es salaam.

“Tumeamua kwa hiyari yetu kutembea kwa miguu na baiskeli kutoka Kahama mpaka Dar es Salaam kumpongeza Rais wetu mpendwa na tunaomba Watanzania wenzetu wanaoipenda nchi yetu watuunge mkono”, alisema Bw. Shami.

Bw. Shami amesema kuwa wachimbaji hao wamefurahishwa na juhudi za serikali ya awamu ya tano pamoja na moyo wa utu wa Mhe. Raisi katika kuhakikisha rasilimali za Tanzania zinawanufaisha Watanzania wote.

“Kuna wakati tulijiona kama yatima kwenye nchi yetu, na tulianza kuamini kuwa dhahabu yetu imegeuka laana badala ya baraka alizotupatia mwenyezi Mungu bure, lakini sasa tunaiona nuru kubwa kupita Raisi wetu”, amesisitiza Bw. Shami.

Aliendelea kusema kuwa mwaka 2008, Shirika la TYHRA kwa kushirikiana na wachimbaji wadogo, wadau wa maendeleo na wafanyakazi wa mgodi wa Bulyanhulu walianzisha  harakati zilizojulikana kama ‘Native Solidarity Movement’ kwa lengo la kudai haki zao za msingi katika migodi lakini hazikuzaa matunda.

 Hata hivyo Bw. Shami ameyaomba mashirika mengine yasiyo ya kiserikali na yeyote anayeitazama Serikali kwa jicho la maendeleo na mwenye mapenzi mema na nchi yake wajaribu kutumia nguvu kubwa kuipongeza, kuishauri na kuitia moyo serikali kama wanavyotumia nguvu kubwa kukosoa na kulaani mambo mbalimbali yanayofanywa na Serikali.

 Bw. Shami alifananisha matatizo na changamoto za Watanzania sawa na kupewa tembo mkubwa kumla, jambo ambalo linahitaji hatua kwa hatua, kipande kwa kipande, hivyo aliwataka Watanzania wampe Rais muda wa kutatua changamoto zao kwani  juhudi zake zimeonekana toka alipoingia madarakani.

Shirika la Young Human Right Advocates linajihusisha na utetezi wa haki za binadamu na wadau wa maendeleo. Shirika hilo linashirikiana na wachimbaji wadogo wa wilaya ya Kahama kuchangia maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa na pia kukemea na kuelimisha jamii.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi