WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wabunifu majengo na wakadiriaji majenziwajiepushe na vitendo vya rushwa ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inalingana na thamani ya fedha inayotumika.
’’Epukeni vitendo vya rushwa ambavyo huisababishia Serikali hasara kubwa na kuleta usumbufu kwa wananchi.Ni matumaini yangu kuwa mtafanya kazi kwa weledi na kufuata maadili ya taaluma zenu’’.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Mei 18, 2018) wakati akifungua semina endelevu ya 29 ya Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi, iliyofanyika Jijini Dodoma.
Amesema wataalamu hao ni vema wakahakikisha majengo wanayobuni yanakuwa bora katika muonekano na mandhari yake iwe yenye kuvutia na yenye kuzingatia utunzaji wa mazingira na matumizi bora na endelevu ya nishati.
Pia Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzikwa kuchagua mada inayohusu jukumu la wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi katika kuendeleza viwanda hapa nchini.
Amesema anatambua kuwa ujenzi wa viwanda unaendana na ujenzi wa miundombinu kama majengo, barabara, madaraja, miundombinu ya nishati na viwanja vya ndege, ambayo ni muhimu katika kuimarisha uchumi wa viwanda.
’’Hivyo, wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi mna mchango mkubwa sana katika kufikia uchumi wa viwanda. Nitoe rai kwa Bodi ihakikishe kuwa miradi yote ya majengo pamoja na miundombinu mingine inashirikisha wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi katika ubunifu na usimamizi wa ujenzi wake.’’
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amezitakataasisi za Serikali na waendelezaji binafsi wahakikishe wanatunza majengo ya kale, kama Sheria ya Mambo ya Kale inavyoelekeza.
Amesema nchi nyingi duniani zinaenzi majengo ya kale, ambayo yanatoa taswira ya nchi husika, ambapo kasi ya ukuaji wa sekta ya ujenzi hapa nchini haiwezi kuondoa dhana hiyo.
’’Kwa msingi huo, napenda kusisitiza kuwa taasisi za Serikali na waendelezaji binafsi, wote wanapaswa kutunza majengo ya kale, kama Sheria ya Mambo ya Kale inavyoelekeza’’.
Waziri Mkuu amesema jambo la muhimu ni kutoa elimu, ili wananchi waelewe umuhimu wa kutunza historia ya nchi yao kwa kupitia majengo ya kale ambayo pia yanaweza kuwa chanzo cha mapato kwa Serikali kupitia sekta ya utalii.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
41193 - DODOMA.
IJUMAA, Mei 18, 2018.