Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Vyombo vya Habari Vyatakiwa Kuendelea Kulinda Amani kuelekea Uchaguzi Mkuu
Aug 19, 2020
Na Msemaji Mkuu

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza na kufurahi na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe.Loata Olesanare wakati wa ziara ya kukagua usikivu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kuzungumza na Wadau wa Sekta ya Habari mkoani hapo Agosti 18, 2020.

Na Shamimu Nyaki –WHUSM

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amevitaka Vyombo vya Habari nchini kuendelea kudumisha na kulinda amani katika kipindi chote cha kampeni mpaka Uchaguzi Mkuu kwa kuandika na kutangazia umma habari ambazo zina ukweli.

Waziri Mwakyembe ameyasema hayo Agosti 18, 2020 alipokua akifanya mahojiano na vyombo vya habari vya redio na runinga vinavyomilikwa na taasisi ya “ISLAMIC FOUNDATION” ambavyo ni redio Imaan na TV Imaan pamoja na kuzungumza na Wadau wa Sekta ya Habari wa Mkoa wa Morogoro ambapo amesema wanahabari wana nafasi ya kulinda au kubomoa amani ya nchi kupitia kalamu zao kama wasipozitumia vizuri, huku akitolea mfano nchi ambazo ziliingia katika machafuko kupitia vyombo vya habari.

“Mwanahabari ni mwalimu, mfasili, mkalimani, mchambuzi na mtetezi hivyo ni vizuri akatumia taaluma yake vizuri katika kuhabarisha umma ili asilete migogoro, Pia mwanahabari anapaswa kuelezea sera za wagombea na vyama vyao ili kuisaidia jamii kutambua mgombea sahihi na kuchagua mgombea bora”, alisema Mhe. Mwakyembe.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akiwa katika mahojiano na kituo cha TV Imaan cha mkoani Morogoro alipotembelea kituo hicho Agosti 18, 2020. Katikati ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Islamic Foundation Bw.Aref Nahd na Kushoto ni mtangazaji wa kituo hicho Bw. Momahed Mattano.

Dkt. Mwakyembe ameongeza kuwa ifikapo mwaka 2021 hakuna Mwandishi wa Habari yoyote ambaye kama atakuwa hajakidhi vigezo vya Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 pamoja na kanuni zake za mwaka 2017 ataruhusiwa kufanya kazi ya uandishi wa habari, lengo likiwa ni kuifanya taaluma hiyo kutambulika na kuheshimika.

Katika hatua nyingine Waziri huyo alipozungumzia usikivu wa Shirika la Utangazaji Tanzania TBC amesema kwamba Serikali imeimarisha usikivu wa shirika hilo ambapo mpaka sasa usikivu ni zaidi ya asilimia 70 na matarajio ni kufikia maeneo yote ndani ya mwaka huu wa fedha.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Isamic Foundation ya mkoani Morogoro Bw.Aref Nahd wakati Mhe.Waziri alipotembelea taasis hiyo Agosti 18, 2020.

Kwa upande wake Mhandisi Mkuu wa Shirika hilo, Bibi. Upendo Mbelle amesema katika kuimarisha usikivu wa TBC mkoani Morogoro Shirika linajenga kituo eneo la Kisaki na kuweka mtambo wa Kilo Wati moja (KW 1) ambacho kikikamilika mkoa wote utasikika, huku akeleza kuwa eneo la Mlimba litawekwa mtambo ambao tayari umeshaagizwa na mkandarasi ameanza kufanya kazi.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bw. Bakari Msolwa akizungumza katika mkutano wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Dkt. Harrison Mwakyembe (wa pili kushoto) Agosti 18, 2020.

“Morogoro ina changamoto ya milima na mabonde, lakini tukimaliza kuweka mitambo katika maeneo hayo usikivu hautakuwa na shida tena, na baada ya kazi hiyo tutafunga mtambo mdogo katika Wilaya ya Gairo”, alisema Bibi Upendo.

Vilevile Mkuu wa Mkoa wa Mororgoro Mhe. Loata Olesanare amesema mkoa huo unafanya vizuri katika sekta zote za Wizara hiyo ikiwemo kuhifadhi na kulinda mila na desturi pamoja na kulinda maeneo yote ya kiutamaduni yalipo mkoani hapo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi