Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Vyombo vya Habari Vyashauriwa Kushirikiana na BAKITA Kujua Matumizi Sahihi ya Kiswahili .
Aug 15, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Shamimu Nyaki.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Elisante Ole Gabriel  amevishauri vyombo vya habari  kushirikiana na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kujua lugha sahihi ya Kiswahili wakati wanapofikisha ujumbe wa kwa  jamii .

Ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara katika Kampuni ya  Magazeti ya Mwananchi (MCL) ambapo ameeleza kuwa Baraza la Kiswahili lipo kwa ajili ya kukuza  na kuendeleza Lugha ya Kiswahili hivyo vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika matumizi sahihi ya Kiswahili.

“Vyombo vya habari mna nguvu kubwa kwa jamii na mnafuatiliwa na watu wengi hivyo mnapaswa kujua matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili katika uandishi,utangazaji pamoja na matumizi mengine katika kuwasiliana na hadhira yenu,”alisema Prof. Elisante.

Aidha, ameongeza kuwa ni wajibu kwa wadau wa habari kusoma vizuri  na kuelewa Sheria ya Huduma za Habari na kutambua mambo muhimu yaliyoanishwa katika Sheria hiyo ikiwemo kuwa na Mikataba,Bima ya Afya na Bodi na Mfuko wa Habari utakaowawezesha kupata ufadhili wa kusoma.

Hata hivyo ameipongeza Kampuni ya Mwanachi kwa kuwa na Kitengo cha lugha ya Kiswahili na maktaba nzuri ya kuhifadhi magazeti yote ambayo yameshasomwa na kuvishauri vyombo vingine kuwa na mfumo huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Bw. Francis Nanai  amesema kuwa Kampuni yake itaendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza majukumu yake kwa manufaa ya nchi.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi