Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Vyama vya Wafanyakazi Vyasisitizwa Kuwasaidia Watumishi Kupata Haki Zao
Mar 18, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Jacquiline Mrisho -MAELEZO

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Francis Michael amevisisitiza Vyama vya Wafanyakazi nchini kuendelea kuwasaidia Watumishi kupata haki zao.

Ameyazungumza hayo leo jijiji Dodoma wakati akifungua Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo ambapo alisisitiza kuwa, kuwasaidia Watumishi mahala pa kazi ni wajibu wao.

Akiongelea kuhusu Baraza hilo, Dkt. Michael  amesema kuwa ni jukwaa muhimu kufanyika kwa sababu ndio kiunganishi madhubuti kati ya Menejimenti na Watumishi.

“Mabaraza haya ya Wafanyakazi ni muhimu sana kufanyika, sisi Menejimenti tunakutana kwenye vikao vyetu mara kwa mara lakini mara chache tunapata wasaa wa kuzungumza na Watumishi wetu, hivyo kupitia Mabaraza haya tunazungumza na Watumishi wetu,” alisema Katibu Mkuu, Dkt. Michael.

Aidha, amewasisitiza Wajumbe wanaochaguliwa katika Mabaraz a hayo kuleta mawazo ya Watumishi waliomchagua na sio kuleta mawazo yao peke yao pia, amewakumbusha kurudisha mrejesho kwa Watumishi ili waweze kufahamu na kutekeleza yale waliyokubaliana katika Mabaraza hayo.

Fauka na hayo, Katibu Mkuu amewaahidi Watumishi hao kuwa, Wizara itaendelea kusimamia na kuimarisha maslahi ya Watumishi wake ikiwemo upandishwaji wa vyeo, kuendelea kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi, likizo na haki zingine za Watumishi.

Ili kuleta matokeo chanya, amewataka Watumishi hao kufanya kazi kwa ushirikiano, bidii, uadilifu, kuepuka vitendo vya rushwa pamoja na kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zingine zilizowekwa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi