Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Viwanja vya Ndege 11 Nchini Kufanyiwa Upanuzi na Ukarabati
Feb 05, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Beatrice Lyimo- MAELEZO, DODOMA

Serikali imeanza majadiliano na Benki ya Dunia ili kupata mkopo wa kugharamia ukarabati na upanuzi wa Viwanja vya Ndege 11 kwa kuzingatia mapendekezo ya ripoti ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambao ulizingatia mambo mbalimbali  ikiwa ni pamoja na ukuaji wa shughuli za kiuchumi, utalii na mahitaji ya usafiri wa anga.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano  Mhandisi Atashasta Ndikiye leo Mjini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Tanga Mhe. Mussa Mbarouk lililohusu Ujenzi wa Uwanja wa Ndege mkubwa na wa kisasa katika jiji la Tanga.

Mhandisi Ndikiye amesema kuwa kiwanja cha ndege cha Tanga ni miongoni mwa viwanja hivyo 11 vilivyofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa kugharamiwa na Benki ya Dunia kupitia mradi wa Transport Sector Support Project (TSSP).

"Katika upembuzi huo kiwanja cha ndege cha Tanga ni miongoni mwa viwanja vilivyopewa kipaumbele kwa mahitaji ya ukaribu hivyo katika majadiliano ya awali Benki ya Dunia imeonesha nia ya kugharamia ukarabati wake.”

"Kwa sasa majadiliano kati ya Serikali na Benki ya Dunia yanaendelea yakiwemo mapitio ya awali ya ripoti za miradi iliyopendekezwa pamoja na maandalizi ya taarifa mbalimbali zinazohitajika kabla ya mkataba wa mkopo kusainiwa na baadaye kutangaza zabuni," amefafanua Mhandisi Ndikiye.

Hata hivyo, Mhandisi Ndikiye alivitaja viwanja vingine vilivyofanyiwa upembuzi yakinifu  ikiwemo Lake Manyara, Musoma, Iringa, Songea, Kilwa Masoko, Lindi, Moshi, Njombe, Simiyu na Singida ambapo usanifu huo ulimalizika mwezi June 2017 kwa kuhusisha usanifu wa miundombinu ya viwanja  hivyo kwa ajili ya upanuzi na ukarabati ili kukidhi mahitaji ya sasa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi